Yeye ndiye Allah, Mwenyezi Mungu, aliye kuumbeni hapo mwanzo kwa nafsi moja. Na akajaalia katika nafsi ile ile mwenzie, na vizazi vyao vikaendelea kuwepo. Nanyi mlikuwa mume na mke. Basi alipo muingilia akachukua mzigo mwepesi, nayo ndio mimba changa, inapo kuwa kama pande la damu na pande la nyama. Mimba ikiwa nzito katika tumbo lake huyo mke, mume na mke humwomba Mola wao Mlezi wakisema: Wallahi, ukitupa mwana mzima asiye na ila katika umbo lake, tutakushukuru kwa neema yako.