Hao walio majeuri na wakapanda kiburi katika ardhi wakakataa kukubali yaliyo sawa bila ya haki, nitawazuia wasiweze kuzizingatia dalili za uwezo wangu ziliomo katika nafsi za watu na jiha zote. Watu hawa hata wakiona kila Ishara inayo thibitisha ukweli wa Mitume wetu hawaisadiki. Na wakiiona njia ya uwongofu hawaipiti, na wakiiona njia ya upotofu ndio wanaipita! Hayo yanatokea kwao kwa sababu wamezikanusha Ishara zetu zilio teremshwa, na wameghafilika na kuongoka kwazo.