Ili kuwanabihisha njia ya maumbile ya kisharia, Nabii wa Mwenyezi Mungu Luut'i akasema: Hawa mabinti wa mji huu, nao ni binti zangu, waoeni ikiwa mnataka kukidhi matamanio yenu.
Ewe Nabii Muaminifu! Naapa kwa haki ya uhai wako! Hawa wamo katika mghafala, hawajui yatakayo wateremkia. Wamekuwa kama walio lewa! Hakika wao wamo katika upotovu, wanatapatapa, hawajui wapite wapi.
Mwenyezi Mungu Aliye takasika katekeleza hukumu yake, akasema: Miji yao tukaifanya juu chini kwa kuivuruga, na tukawateremshia udongo ulio fanyika mawe ukiwateremkia kama mvua. Majumba yao yakaporomoka. Na wakitoka nje hukuta hiyo mvua ya mawe. Kwa hivyo wakawa wamezungukwa kila jiha. (upande)
Haya yaliyo washukia kaumu Luut'i ni alama wazi ya kuonyesha vipi Mwenyezi Mungu Mtukufu anavyo timiza ahadi yake. Wajuao mambo wanayatambua hayo, na wanayaelewa matokeo yake kwa alama zake, kwani kila kitendo chenye sifa ya ukosefu kina alama yake isiyo potea. Matokeo yake ni mfano wa haya, duniani na Akhera.
Kama kaumu ya Luut'i walivyo kadhibisha, kadhaalika wakaazi wa Kichakani kwenye msitu wenye matunda walimkanya Mtume wao. Wakawa madhaalimu wenye kudhulumu mno katika imani yao na maingiliano yao.
Na kama walio tangulia hali kadhaalika wakaazi wa Hijr walimkanusha Mtume wao aliye tumwa kwao, na kwa hivyo wakawa wamewakanusha Mitume wote. Kwani ujumbe wa Mwenyezi Mungu ni mmoja. Watu wa Hijr ndio Thamud. Na Hijr ni bonde baina ya Madina na Sham. Tazama maelezo juu ya Aya 73 ya Surat Al-Aa'raaf.
Nao walikuwa watu wenye nguvu na wajenzi. Walikuwa wakijenga majumba yao katika milima na wakiichonga hiyo hiyo milima. Na wao walikuwa wakijiamini kuwa wametua na nafsi zao na mali yao.
Hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyo kati yao katika anga, na viliomo ndani yake, watu na wanyama, na mimea na visio na uhai, na vinginevyo ambavyo mwanaadamu havijui, isipo kuwa kwa uadilifu, na hikima, na maslaha ambayo hayaambatani na fisadi ya kudumu isiyo na mwisho. Na kwa hivyo basi ni lazima siku ya kukomesha shari ifike bila ya shaka yoyote. Basi ewe Nabii Mtukufu! Wasamehe hao washirikina adhabu ya duniani, na ingiana nao kwa kuwastahamilia maudhi yao. Na kuwaita wito kwa hikima ni kuingiliana kwa usamehevu na upole.
Ewe Nabii Muaminifu, tumekupa Aya saba za Qur'ani, nazo ni Sura ya Al- Fatiha unayo ikariri katika kila Swala, na humo yamo ya kutunyenyekea na maombi ya uwongofu yaliyo kaamili. Na tumekupa Qur'ani Tukufu yote. Na ndani yake mna hoja, na miujiza. Kwa hivyo wewe una nguvu ambazo zinakufalia usamehe.
Ewe Mtume! Usivitazame kwa kuvitamani na kuvitaka vitu vya starehe ya dunia tulivyo wapa makafiri wa kishirikina, na Kiyahudi, na Kikristo, na Kimajusi. Kwani hivyo ni duni kwa kulinganisha na ulio pewa wewe katika kuwasiliana nasi, na Qur'ani Tukufu. Wala usiwasikitikie kwa sababu ya kuendelea kwao na madhambi. Nawe tulia, na unyenyekee, na wachukue Waumini ulio nao kwa upole. Kwani hao ni nguvu za Haki, na watu wa Mwenyezi Mungu.