Tukamwambia Adam na mkewe na vizazi vyao vijavyo na Iblis: Shukeni katika Ardhi, na huko mtalazimishwa mambo. Yakikujieni hayo kutokana na Mimi - na hapana shaka yatakujieni - basi wale watakao itikia amri yangu, na wakafuata uwongofu wangu hawataona khofu yoyote, na hawatopata huzuni, kwa kukosa thawabu, kwa sababu Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa atendaye mema.
Na wale ambao watapinga na watawakanusha Mitume wa Mwenyezi Mungu na Vitabu vyake, hao ni watu wa Motoni, watabaki huko milele, wala hawatatoka wala hawatakufa.
Enyi Wana wa Israili kumbukeni neema zangu nilizo kutunukieni nyinyi na wazee wenu kwa kuzifikiri na kushukuru na kutimiza agano langu nililo lichukua kwenu, na nyinyi nafsi zenu mkalikiri, nalo ni Imani, na Vitendo vyema, na kuwasadiki Manabii wajao baada ya Musa, ili Nami nitimize ahadi yangu kwenu, nayo ni kukulipeni malipo mema, na neema ya kudumu. Na wala msimwogope mtu yeyote isipo kuwa Mimi, na tahadharini na kufanya mambo yatakayo nifanya nikasirike nanyi. Aya hii inaonyesha kuwa ahadi, au agano, ni waajibu wa pande zote mbili zilizo ahidiana kutimiza lilio lazimika. Akiacha mmojapo basi haimlazimu wa pili kutimiza agano lake.
Na isadikini Qur'ani iliyo teremshwa kusadikisha vile vitabu mlivyo navyo, na kufunza Tawhidi (kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja) na kumwabudu Mwenyezi Mungu, na uadilifu baina ya watu. Wala msikimbilie kutaka kuipinga Qur'ani msije mkawa ndio wa mwanzo kuikana, na ilhali ifaavyo ni nyinyi ndio muwe wa mwanzo kuiamini. Wala msiziache Ishara za Mwenyezi Mungu mkenda badala yake mkachukua chenginecho kipitacho njia katika starehe za uhai wa dunia. Na niogopeni Mimi tu, na fuateni Njia yangu, na wacheni upotovu.
Wala msichanganye Haki iliyo toka kwangu na upotovu mlio uzua nyinyi, hata ikawa halijuulikani la kweli na la uwongo. Wala msiifiche Haki, na katika hiyo Haki ni kumsadiki Muhammad, na nyinyi mnajua kuwa yeye ni wa kweli na wa kusadikiwa.
Itikieni Imani. Shikeni Swala yenye nguzo zilizo simama baraabara. Na toeni Zaka muwape wanao stahiki. Na salini pamoja na jamaa wa Kiislamu ili mpate malipo ya Swala na thawabu za kusali jamaa. Na haya yanalazimu kuwa muwe Waislamu.
Je, mnawataka watu wafanye kheri, na wajilazimishe ut'iifu, na waache maasia, kisha nyinyi hamtendi myasemayo, wala hamjilazimishi nafsi zenu kwa yale myatakayo? Kwa hivi mnajipoteza nafsi zenu, kama kwamba mmezisahau, na ilhali nyinyi mnasoma Taurati na ndani yake pana maonyo na mikemeo kwa mwenye kusema asilo litenda. Basi nyinyi hamna akili ya kukuzuieni na kwenda mwendo huu wa kutukanisha?
Na tafuteni msaada wa kutekeleza waajibu kwa subira na kuizuia nafsi isitende yanayo udhi. Katika hayo ni kwa kufunga Saumu, na kwa Swala ambalo ni jambo kubwa lenye kuusafisha moyo na kuzuia kutenda machafu na maovu, na kwa hivyo ndio yakawa mazito ila kwa wenye kupenda ut'iifu ambao nyoyo zao zimetulia kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu.
Hao ndio wanyenyekevu walio tulia nyoyo zao, ambao wanaiamini Siku ya mwisho, na wana yakini kuwa watakutana na Mola wao Mlezi wakati wa kufufuliwa, na kwake Yeye pekee ndio watarejea ili awahisabie kwa yale waliyo yatenda na awalipe kwayo.
Enyi Wana wa Israili! Kumbukeni neema zangu nilizo kuneemesheni kwa kukutoeni katika dhulma ya Firauni, na nikakuongoeni na nikakuwekeni imara katika nchi baada ya kuwa mlikuwa mkionewa humo. Mshukuruni kwa kumt'ii Mwenye kukutunukieni hayo. Na kumbukeni kuwa Mimi niliwapa baba zenu mlio zalikana kutoka kwao nisiyo wapa wowote wengineo wakati wenu. Haya wanaambiwa taifa la Mayahudi walio kuwako zama za Mtume.
Iogopeni Siku ya Hisabu kali, Siku ya Kiyama, siku ambayo hapana mtu ataeweza kumtetea mtu, na wala hapana mtu ataye mfaa mtu, wala hakubaliwi mtu kuleta mwombezi, kama ilivyokuwa hatokubaliwa mtu kutoa fidia ya dhambi, wala hapana mtu ataye weza kuizuia adhabu isimpate mwenye kustahiki.