Mwenyezi Mungu, Subhanahu, Aliye Takasika, amebainisha kuwa ni Yeye ndiye aliyempa uhai mtu, na akamweka duniani. Kisha amebainisha vile vile asli ya kumweka mwanaadamu na ujuzi aliyo mpa, na akakumbushwa hayo. Basi kumbuka, ewe Muhammad, neema nyingine ya Mola wako Mlezi kumpa mtu, nayo ni pale alipo waambia Malaika: Mimi nitajaalia awepo katika ardhi mfwatizi, ambaye nitamweka hapo, na nimpe madaraka, naye ni Adam na vizazi vyake. Mwenyezi Mungu atamweka kama Khalifa, au naibu wa kuimarisha dunia, na kutekeleza amri, na kuzitengeneza nafsi. Malaika wakauliza kutaka kujua nini siri ya hayo, wakasema: Je, utaweka katika Ardhi atakaye leta uharibifu humo kwa maasi, na atakaye mwaga damu kwa uadui na mauwaji kwa kufuata tabia yake ya matamanio, na ilhali sisi tunakutakasa na yasiyo laiki na utukufu wako, na tunasafisha kumbusho lako, na tunakutukuza? Mola wao Mlezi akajibu: Mimi ninajua maslaha ya hayo msiyo yajua nyinyi.
Na baada ya Mwenyezi Mungu kwisha kumuumba Adam na akamfundisha majina ya vitu vyote na sifa zao ili atue katika ardhi na anufaike navyo, aliwaletea hivyo vitu Malaika na akawaambia: Niambieni majina ya vitu hivi na sifa zao kama kweli nynyi ndivyo kama mnavyo dhani kuwa mnastahiki kupewa madaraka katika Ardhi, na kuwa hapana aliye bora kuliko nyinyi kwa sababu ya ut'iifu wenu na ibada zenu.
Malaika wakatambua upungufu wao, wakasema: Sisi tunakutakasa Ewe Mola wetu Mlezi kwa mtakaso ulio laiki nawe. Tunakiri kuwa tumeshindwa, na hatuwezi kupinga. Kwani hatuna ilimu kuliko uliyotupa Wewe, na Wewe ndiye Mjuzi wa kila kitu, na Mwenye hikima na hukumu katika kila jambo ulitendalo.
Mwenyezi Mungu alimwambia Adam: Watajie Malaika khabari za vitu hivi. Akataja; na ukadhihiri ubora wake juu yao. Na hapo Mwenyezi Mungu akawaambia kuwakumbusha vipi ujuzi wake ulivyo enea: Sikukwambieni kuwa Mimi ninajua siri za mbingu na ardhi, na hapana ajuae hayo isipo kuwa Mimi, na Mimi ninajua mnayo yadhihirisha katika kauli yenu, na mnayo yaficha katika nafsi zenu.
Na kumbuka Ewe Nabii! Tulipo waambia Malaika: Mnyenyekeeni Adamu kwa kumwamkia na kuukiri ubora wake. Wakat'ii Malaika wote ila Iblis. Yeye alikataa kusujudu akawa miongoni mwa walio asi, walio zikataa neema za Mwenyezi Mungu, na hikima yake, na ujuzi wake.
Kisha Mwenyezi Mungu alimuumba Adam na mkewe, na akawaamrisha wakae katika Bustani ya neema. Akamwambia: Kaa wewe na mkeo katika Bustani hii na kuleni humo mtakavyo vya kutosha bila ya kutaabika, na kaeni mtakapo, mle mtakacho. Lakini Mwenyezi Mungu aliwatajia mti maalumu na akawahadharisha wasiule, na akawaambia: Msiukaribie mti huu, wala msile matunda yake. Mkifanya hivyo mtakuwa miongoni mwa walio dhulumu, na mtakuwa waasi.
Lakini Iblis, anaye mhusudu na kumchukia Adam, alimfanyia vitimbi, akawadanganya mpaka wakateleza wakala mti walio katazwa. Mwenyezi Mungu akawatoa katika ile neema na ukarimu walio kuwa nayo. Mwenyezi Mungu Mtukufu akawaamrisha washukie kwenye Ardhi waishi humo wao na vizazi vyao, na wawe na uadui baina yao kwa wao kwa sababu ya ushindani na kupotozwa na Shetani. Na huko kwenye Ardhi pawe pahali pa kukaa kwao na kupata maisha, na kustarehe kutako kwisha kwa kutimia wakati.
Adam na mkewe walitambua makosa yao na kujidhulumu nafsi zao. Mwenyezi Mungu Mtukufu alimfunza Adam baadhi ya maneno ya kutubia na kuomba msamaha na akayasema. Mwenyezi Mungu alimkubalia toba yake, na akamsamehe, kwani Yeye ni mwingi wa kukubali toba, naye ni Mwenye kuwarehemu waja wake wanyonge.