Hii ndiyo hali ya waongofu. Ama wajinga, majaahili, walio acha kujitayarisha kwa Imani kwa mapuuza na kufanya inda, wasimwitikie Mwenyezi Mungu, basi ni sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye.
Ukafiri umesaki kwa watu hao, hata imekuwa kama nyoyo zao zimetiwa muhuri, zimezibwa kwa vizibo, haziingii kitu chochote zaidi ya kiliomo ndani yake. Na kama kwamba masikio yao pia yamezibwa, hayasikii onyo lake la kweli, na kama kadhaalika wamefunikwa kwa vitanga vya macho. Hawazioni ishara za Mwenyezi Mungu zenye kuonyesha Imani. Kwa hivyo basi imekuwa wanastahiki kuwafikilia adhabu iliyo kali.
Na miongoni mwa makafiri wapo watu ambao husema kwa ndimi zao yasiyo kuwamo nyoyoni mwao. Hudhihirisha imani na kusema: "Sisi tunamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Kiyama," na wala hawasemi kweli. Basi hao hawaingii katika kundi la Waumini.
Hao makafiri wadanganyifu huwakhadaa Waumini kwa wanayo yafanya, na wao hudhania kuwa wanamdanganya Mwenyezi Mungu. Wanafikiri kuwa Yeye hayajui wanayo yaficha, na kumbe Yeye anayajua ya siri na yanayo non'gonwa. Basi wao kwa hakika wanajikhadaa wenyewe, kwa sababu madhara ya vitendo vyao yatawapata wao, sasa au baadae. Mwenye kumkhadaa mtu, na akadhani kuwa huyo mtu hajui naye kumbe anajua, basi inakuwa anajikhadaa mwenyewe nafsi yake.
Katika nyoyo za watu hawa mna maradhi ya uhasidi na chuki kwa watu wenye imini, na itikadi zao zimefisidika. Mwenyezi Mungu basi anawazidishia hayo maradhi yao, kwa ajili ya kuinusuru Haki, kwani hayo yanawaudhi wao kwa sababu ya uhasidi wao, na chuki yao, na inadi yao. Watu hao watapata adhabu iliyo chungu Duniani na Akhera kwa sababu ya uwongo wao na upinzani wao.
Na pindi mmojawapo wa walio ongoka akiwaambia hawa wanaafiki: "Msifanye uharibifu katika nchi kwa kuipinga Njia ya Mwenyezi Mungu, na kueneza fitna, na kuwasha moto wa vita," wao hujitoa makosani mwa uharibifu, na husema: "Kee sisi ndio tunao tengeneza." Na hayo ni kwa kuwa ghururi yao imepita mpaka. Huu ndio mwendo wa kila mharibifu, khabithi mwenye ghururi. Yeye hudai kuwa ule uharibifu wake ndio matengenezo na maendeleo.
Enyi Waumini! Amkeni, mtanabahi, muwatambue kuwa hao ndio mafisadi wa kweli, lakini wenyewe hawautambui ufisadi wao kwa ajili ya ghururi walio nayo, wala hawaitambui adhabu kali watakayo ipata kwa unaafiki wao huu.
Akitokea mtu kuwanasihi na kuwaongoza kwa kuwaambia:"Kubalini yalio waajibu." Nako ni kuwa muamini Imani safi kama wanavyo amini watu wakamilifu wanao itikia wito wa akili, wao hufanya maskhara na kejeli na husema: "Si laiki yetu sisi kuwafuata hawa wajinga, wapungufu wa akili." Mwenyezi Mungu anawarudi kwa ule ubishi wao na kuwahukumia kuwa ni wao tu ndio wajinga, wapumbavu, lakini wao hawajui kwa ujuzi wa yakini kuwa ujinga na kukosa kuelewa ni kwao wao tu.
Hawa wanaafiki wakiwakuta Waumini wa kweli husema: "Sisi tunaamini hayo hayo mnayo amini nyinyi," yaani kumkubali Mtume na wito wake, "na sisi tu pamoja nanyi katika itikadi." Wakisha ondoka wakakutana na wenzao wanao shabihiana na mashetani kwa fitina na ufisadi, huwaambia: "Sisi tu pamoja nanyi katika njia yenu na kazi yenu, lakini tukiwaambia yale hao Waumini kwa ajili ya kuwalazia na kuwadhihaki tu."
Mwenyezi Mungu Subhana atawalipa kwa huko kudhihaki kwao, na atawaandikia uangamifu unao lingana na hayo maskhara yao na dharau zao. Atawatendea inavyo stahili kutendewa mwenye kudhihaki, na anawapa muhula tu katika dhulma yao iliyo ovu, inayo watia upofu wasiione haki. Kisha khatimaye ndipo atapo watia mkononi kwa adhabu yake.
Na hawa (wanaafiki) kwa kukhiari upotofu badala ya uwongofu wamekuwa kama mfanya biashara aliye khiari kwa biashara yake bidhaa mbovu ya kuchina, basi hafanikiwi kupata faida yoyote. Hupoteza rasilmali yake. Na wao basi hawaongokewi katika 'amali yao.