Waambie: Mimi siimilikii nafsi yangu kujiletea nafuu, wala kujikinga na madhara, ila Mwenyezi Mungu akipenda hayo. Hapo ndio hunipa mamlaka. Na lau kuwa mimi najua yale yaliyo fichikana kwangu, kama mnavyo dhani, basi ningeli kithirisha kila kheri, kwa kuwa ninajua sababu zake. Na ninge ilinda nafsi yangu na kila ovu, kwa kuyaepuka yanayo leta madhara. Mimi si chochote ila ni mwonyaji wa adhabu, na mbashiri wa thawabu, kwa kaumu wanayo iamini Haki na wanait'ii.
Yeye ndiye Allah, Mwenyezi Mungu, aliye kuumbeni hapo mwanzo kwa nafsi moja. Na akajaalia katika nafsi ile ile mwenzie, na vizazi vyao vikaendelea kuwepo. Nanyi mlikuwa mume na mke. Basi alipo muingilia akachukua mzigo mwepesi, nayo ndio mimba changa, inapo kuwa kama pande la damu na pande la nyama. Mimba ikiwa nzito katika tumbo lake huyo mke, mume na mke humwomba Mola wao Mlezi wakisema: Wallahi, ukitupa mwana mzima asiye na ila katika umbo lake, tutakushukuru kwa neema yako.
Akisha wapa wakitakacho, huwafanya masanamu ndio washirika wa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika ile zawadi yake ya ukarimu, kwa kuyatambikia kama kwamba ndio wanayashukuru. Na Mwenyezi Mungu pekee ndiye anaye stahiki kushukuriwa. Yeye ametukuka, hawezi kuwa kama hiyo miungu yao ya kishirikina.
Na nyinyi mnao yaabudu masanamu! Mkiyaomba hayo masanamu yakuongozeni mpate mnacho kipenda hayakuitikieni hayo myatakayo! Ni sawa sawa kwenu kuwa hapana faida ya kuwaomba au mkinyamaza. Hali yao haibadiliki vyo vyote vile.
Hakika hao mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu, na mkataraji nafuu kwao, wao wenyewe wanamnyenyekea Mwenyezi Mungu kwa hukumu ya maumbile yao. Kwani Yeye Mwenyezi Mungu amewafanya wafuate amri yake mfano wenu nyinyi. Kama nyinyi mnasema kweli katika madai yenu kuwa hao wanaweza lolote, basi watakeni, na wao wakutimilizieni.
Bali haya masanamu ni duni kuliko nyinyi kwa kuumbwa na kuwa! Kwani wao wana miguu ya kuendea? Au wana mikono ya kukinga madhara yasikupateni au yasiwapate wenyewe? Au wana macho ya kuonea? Au masikio ya kusikia hayo mnayo yataka wakakupeni? Hawana chochote katika hayo! Vipi basi mnawashirikisha hao na Mwenyezi Mungu? Na ikiwa nyinyi mnadhani kuwa hio miungu ya uwongo inaweza kunidhuru mimi au mtu yeyote, basi iiteni, na mfanye njama zenu pamoja nao kama mtakavyo, bila ya kunipa muhula wala kungoja. Hao hakika hawawezi kitu! Basi msiningojee, na wala mimi siwabali.