Na kumbukeni kuwa Mwenyezi Mungu amekujaalieni ndio wa kurithi nchi ya A'ad, na akakupeni katika hiyo nchi makaazi mema, mkijenga majumba ya fakhari katika nyanda zake. Na mkichonga milima mkifanya majumba. Basi kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu Mtukufu, alivyo kuwekeni kwa makini katika nchi, wala msifanye maovu katika nchi, mkawa wenye kufisidi na kuharibu baada ya kukaa kwa makini kama huku.
Wale wenye kiburi katika watu wa mbele-mbele na uwongozi waliwasemeza wanyonge kwa kuwalaumu na kuwadhalilisha: Hivyo nyinyi mnaitakidi kuwa kweli Swaleh ametumwa na Mola Mlezi wake? Watu wa Haki wakawajibu: Sisi tunaitakidi na tunakubali aliyo tumwa kwetu.
Inda ya wenye kiburi ikakakamia, na wakampinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakamchinja Ngamia. Walivuka mpaka katika kiburi chao, wakaitupilia mbali amri ya Mola wao Mlezi, na wakasema kwa upinzani: Ewe Swaleh! Tuletee hiyo adhabu uliyo tuahidi ikiwa kweli wewe ni miongoni ya alio watuma Mwenyezi Mungu.
Tetemeko la nguvu lilikuja kuwanyakua, na kulipo pambazuka wakawa wote wamekwisha jifia majumbani mwao wamejifudikiza kifudifudi.
Na kabla ya kuwateremkia adhabu hiyo ndugu yao Swaleh aliwaachilia mbali (kwa kukata tamaa nao), akawaambia: Enyi watu wangu! Mimi nimekufikishieni amri na makatazo ya Mola Mlezi wangu. Na nimekusafieni nasaha yangu, lakini nyinyi kwa ushindani wenu na ushupavu wenu, mmekuwa hamumpendi anaye kunasihini!
Na hakika tulimtuma Nabii wa Mwenyezi Mungu, Lut', kwa kaumu yake; awaite wafuate Tawhidi, yaani ibada ya Mwenyezi Mungu mmoja. Na awazindue juu ya waajibu wa kuachana na makosa maovu kabisa waliyo kuwa wakiyafanya. Aliwaambia: Nyinyi mnakwenda kufanya jambo lilio pita mpaka kwa ubaya wake, kinyume na maumbile? Mmezua uchafu huo ambao unapingana na khulka, na ambao hapana watu walio kutangulieni walio fanya hayo!
Na jambo hilo ni kuwa mnawaendea wanaume kwa kuwatamani, na mnawawacha wanawake! Nyinyi kwa jambo hili inakuwa mnafanya fujo, na mmetoka nje ya maumbile, na mmefanya kitendo asicho fanya hata mnyama.