Hii ni khabari ya Shua'ib katika wito wake kuwalingania kaumu yake. Ama hao kaumu yake walikuwa wamemili juu ya upotovu. Na wale wakubwa wao walio takabari waliukataa wito, na wakaona ni uvunjifu kuifuata Haki. Wakamkabili Shua'ib kumwambia dhamiri yao kwa kusema: Hakika hapana vingine ila tukutoe wewe na hao walio amini pamoja nawe katika mji wetu. Na tutakufukuzeni, wala hamtasalimika na adhabu hii ila mkirejea katika hii dini yetu mliyo iacha. Shua'ib a.s. akawajibu kwa kusema: Turejee katika mila yenu na hali sisi tunaichukia kwa uharibifu wake? Hayawi hayo abadan!
Akaendelea zaidi kuwavunja tamaa yao ya kuwarejeza kwenye mila yao kama walivyo taka. Akasema: Tutakuwa tunamzulia uwongo Mwenyezi Mungu tukiwa katika mila yenu baada ya Mwenyezi Mungu kesha tuhidi kwenye Njia Iliyo Nyooka. Na haifai sisi kuwa katika mila yenu kwa khiari yetu na kutaka kwetu, ila akipenda Mwenyezi Mungu turejee katika mila yenu. Na hayo hayawi! Kwa sababu Mola Mlezi wetu anatujua vyema, na Yeye hataki turejee kwenye upotovu wenu. Yeye aliye tukuka shani yake amekienea kila kitu kwa ujuzi wake. Anatuongoa kwa upole wake na hikima yake kwenye jambo litalo tuhifadhia Imani yetu. Kwa Yeye peke yake ndio tumesalimisha mambo yetu, na huku tunashikilia yale aliyo tuwajibisha tuyashike. Ewe Mola Mlezi wetu! Tutenge sisi na hao kaumu yetu kwa Haki, kama ilivyo kuwa mwendo wako unavyo amua baina ya wenye kufuata Haki na wakatenda mema, na wale wapotovu waharibifu. Na Wewe kwa kuwa ujuzi wako na uwezo ulivyo enea ndiye Muadilifu na Muweza kuliko mahakimu wote.
Hapo basi wale watu walikata tamaa ya kuwafanya Shua'ib na walio kuwa naye wawafuate wao. Na wakajua kuwa hakika hao walikuwa wamethibiti katika Dini yao. Kadhaalika waliogopa wasizidi kuwa wengi wale walio hidika pamoja na Shua'ib kwa kudhihiri nguvu zake na kuthibiti kwake juu ya wito wake. Kwa hivyo wale waheshimiwa wa kikafiri wakawaelekea wafwasi wao wakiwatisha kwa kusema: Wallahi! Mkimfuata Shua'ib mkakubali wito wake, basi hapana shaka nyinyi utakutokeni utukufu wenu na utajiri wenu kwa kufuata dini potovu wasio kuwa wakiifuata wazee wenu.
Basi hapo kauli ya kuteremka adhabu ikawa imethibiti. Wakasibiwa kwa tetemeko lilio tikisa nyoyo zao, wakawa katika majumba yao wamesinukia kifudifudi hawana tena uhai.
Hii ndio shani ya Mwenyezi Mungu na hao walio mkanusha Shua'ib, na wakamtishia, na wakamwonya kuwa watamfukuza katika mji wao, na wakafanya kila kitu kuupinga wito wake. Wamehiliki wao na ukahiliki mji wao, ikawa kama kwamba humo hawakuwahi kuishi wale walio mkadhibisha Shua'ib na wakadai kuwa ati atakaye mfuata atakuwa amekhasiri, na wakatilia nguvu madai hayo. Na lililo kuwa ni kuwa wao ndio walio poteza neema yao ya dunia na Akhera.
Shua'ib alipo ona hilaki ya kuvuruga iliyo wateremkia wale watu, basi aliwaachilia mbali, na akasema kujivua nafsi yake asiwe mkosa pamoja nao: Mimi nimekufikishieni ujumbe wa Mola wenu Mlezi unao pelekea mpate wema nyinyi, lau kuwa mngeli ufuata. Na mimi nimefanya ukomo wa uwezo wangu katika kukunasihini, na kukuwaidhini kwa mambo ya kukuokoeni na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Basi vipi tena niwasikitikie mno watu makafiri? Hayawi hayo baada ya kuwa mimi nimekwisha jiudhuru kwao, na nikatumia juhudi yangu kwa ajili ya kutaka kuwahidi na kuwaokoa, na wao wakakhiari kufuata yale yale ya kuwahiliki.
Na Sisi hatukumpeleka Nabii yeyote kwenye mji akawalingania watu wake wafuate Dini ya Mwenyezi Mungu iliyo sawa, na wao wakakataa kuukubali huo wito, ila tuliwapatiliza kwa ufakiri na maradhi, ili wapate kuwa wanyonge na wamwombe Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu, na kumsafia niya wapate kuondokewa na balaa na wamuitikie Mtume wake.
Basi tena ilivyo kuwa hawakufanya hayo, bali wakaendelea na ukafiri wao na inadi yao, tukawapa mtihani wa kuwapa neema badala ya dhiki ili kuwapururia tu. Tukawapa kutononoka, na nafasi nzuri, na siha na afya, mpaka wakawa wengi, na mali yao yakazidi, wakasema kwa ujinga wao: Hayo yaliyo wapata baba zetu ya mahna, na balaa, na starehe na neema - hayo yote ndio shani ya ulimwengu. Shida na neema huwajia watu kwa zamu. Hawakuzindukana wakajua kuwa haya ni malipo ya kufru zao wakajizuia! Na kwa hivyo wakawa hawaujui mwendo wa Mwenyezi Mungu, iliyo tukuka shani yake, katika sababu za matengenezo na uharibifu wa binaadamu, na nini linalo leta neema na nini linalo leta dhiki! Matokeo ya hayo ni kuwa Mwenyezi Mungu aliwapatiliza kwa kuwaletea adhabu ya kuteketeza kwa ghafla, na wao bila ya kujua nini litawafika.