Hakika Sisi tumekufunulia wewe, ewe Nabii! (tumekuteremshia Wahyi), Qur'ani na Sharia, kama tulivyo wafunulia kabla yako Nuhu na Manabii wa baada yake, na kama tulivyo wapa Wahyi Ibrahim, na Ismail, na Is-haq, na Yaakub, na wajukuu zake, nao wale walio kuwa Manabii wa Mwenyezi Mungu miongoni mwa dhuriya (wazao) wa Yaakub, na Isa, na Ayubu, na Yunus, na Haarun, na Suleiman, na kama tulivyo mfunulia Daud tukamteremshia Kitabu cha Zabur.
Kadhaalika tumewatuma Mitume wengi ambao tumekwisha taja khabari zao kabla yake. Na Mitume wengine hatukukusimulia hadithi zao. Na njia ya kumpa Wahyi Musa ilikuwa Mwenyezi Mungu akisema naye moja kwa moja nyuma ya pazia, lakini bila ya kuwepo mwengine kati.
Tuliwapeleka Mitume hao kuwapa bishara njema ya thawabu wenye kuamini, na kuwaonya adhabu wale walio kufuru, ili watu wasiwe na hoja ya kumtafutia kisababu Mwenyezi Mungu baada ya kwisha wapeleka Mitume. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu, ni Mshindi, wala hana yeyote madaraka pamoja naye, na ni Mwenye hikima kwa atendayo.
Lakini ikiwa hao watu hawashuhudii kukusadikisha, basi Mwenyezi Mungu Mwenyewe anashuhudia kuwa aliyo kuteremshia ni sahihi. Hakika Yeye amekuteremshia hayo kwa hikima, na kwa mujibu wa ujuzi wake. Na Malaika nao wanashuhudia hayo kadhaalika. Na ewe Mtume! Yakutosha wewe ushahidi wa Mwenyezi Mungu, kuliko ushahidi wowote mwenginewe.
Hakika wale ambao wamekufuru wasikusadiki wewe, na wakawazuia watu wasiingie katika Dini ya Mwenyezi Mungu, bila ya shaka wamekuwa mbali mno na Haki.
Wale walio kufuru, na wakajidhulumu nafsi zao, na wakamdhulumu Mtume kwa kuupinga ujumbe wake, na wakawadhulumu watu walipo wafichia Haki, Mwenyezi Mungu hatowasamehe kamwe maadamu watabaki katika ukafiri wao. Wala hatawapa uwongofu wa kuijua njia ya kuvuka. Sio mtindo wake Subhanahu kuwasamehe watu kama hao nao wangali kubaki katika upotovu wao.
Lakini atawapeleka kwenye njia ya Motoni, na humo wabakie daima dawamu. Na hilo kwa Mwenyezi Mungu ni jambo jepesi.
Enyi watu! Amekwisha kukujieni Mtume huyu, Muhammad, na Dini ya Haki kutokana na Mola Mlezi wenu. Basi yaaminini aliyo kuja nayo; ndiyo itakuwa kheri yenu. Na pindi mkikataa ila kukufuru tu, basi mjue kwamba Mwenyezi Mungu ni Mkwasi na imani yenu, hana haja nayo. Yeye ndiye Mwenye kukumilikini nyinyi. Kwani vyote viliomo katika mbingu na katika ardhi ni vyake Yeye, kwa kuvimiliki, kuviumba na kuviendesha atakavyo. Naye ni Mwenye kuvijua vyema viumbe vyake, ni Mwenye hikima katika uendeshaji wake. Haupotezi ujira wa mwema, wala hapuuzi kumlipa mwovu.