Na unapo hukumu baina ya watu muelekee Mwenyezi Mungu, na ukumbuke utukufu wake, na uombe maghfira yake na rehema yake. Kwani kughufiria na kurehemu ndio shani yake Subhanahu wa Taa'la.
Wala usiwatetee wale wanao fanya khiana, na wakaendelea mno katika kuificha hiyo khiana katika nafsi zao. Kwani Mwenyezi Mungu hampendi ambaye mtindo wake ni khiana na kufanya madhambi.
Wanajificha, na wanataka kujisitiri kwa watu wasiione khiana yao. Wala hayumkini kuzificha khiana zao kwa Mwenyezi Mungu, na ilhali Yeye daima yu pamoja nao. Na wao usiku usiku hukubaliana kwa maneno yasiyo mridhi Mwenyezi Mungu ya kuwasingizia tuhuma watu wasio na makosa. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu anajua vyema, na hapana kitu kinacho weza kujificha na ujuzi wake.
Ikiwa nyinyi mnawatetea hao wakosa wasipate adhabu ya duniani, basi hatopatikana wa kuwatetea Siku ya Kiyama mbele ya Mwenyezi Mungu na kukubali kuwa ni mlinzi wao wa kuwasaidia.
Mlango wa toba, hakika, uwazi. Anaye tenda kitendo kiovu cho chote, au akajidhulumu nafsi yake kwa kufanya maasi, kisha akamtaka msamaha Mwenyezi Mungu Mtukufu, atamkuta Mwenyezi Mungu yu tayari kukubali toba yake, na kumghufiria madhambi yake. Kwani ndio mwendo wake Mwenyezi Mungu kughufiria na kurehemu.
Hakika madhara ya madhambi ni juu ya yule yule ayatendayo. Mwenye kuchuma madhambi basi anajidhuru mwenyewe. Na alitendalo linamuangukia mwenyewe. Na Mwenyezi Mungu Aliye takasika na kutukuka anajua aliyo yatenda, na atamchukulia kwa mujibu wa hikima yake. Atamuadhibu au atamsamehe kwa mujibu wa hikima yake.
Na mwenye kutenda makosa na madhambi kisha akamsingizia mwenginewe asiye na kosa alilo litenda - kama vile mwizi kaiba kitu kisha akamsingizia wizi mtu mwengine - mtu huyo ana dhambi mbili. Moja ni uwongo na uzushi, na la pili lile kosa lilio wazi la kuiba.
Lau kuwa Mwenyezi Mungu hakukufadhili kwa kukuteremshia Wahyi, Ufunuo, na akakupa rehema ya kutambua na kufahamu hakika, kikundi cha wapotovu kingependa kukupoteza. Lakini hawapotezi ila nafsi zao. Kwani Mwenyezi Mungu ni muangalizi wako, na ndiye mwenye kukuonyesha haki. Hayakufikilii madhara ya mipango yao na upotezi wao. Yeye Mwenyezi Mungu amekuteremshia Qur'ani Tukufu ambayo hiyo ndiyo mizani ya haki, na ameutuza moyo wako kwa hikima, na amekufundisha Sharia na hukumu ambazo ulikuwa hukuzijua ila kwa kufunuliwa na Yeye. Hakika fadhila za Mwenyezi Mungu juu yako daima ni kubwa.