Hao ndio alio watupa Mwenyezi Mungu na akawafukuzilia mbali kutoka kwenye rehema yake. Na mwenye kutupwa na Mwenyezi Mungu na akatolewa kwenye rehema yake basi kabisa huyo hana wa kumnusuru na kumlinda na ghadhabu ya Mola wake Mlezi.
Hao wamekoseshwa neema ya kuifuata haki, kama walivyo koseshwa na utawala. Na lau wakipewa utawala hawanufaishi watu hata chembe.
Na vipi watu hawa wanavyo waonea maya Waarabu? Na wakaona ni jambo kuu kuwa Mwenyezi Mungu alivyo wapa fadhila yake kwa kuwatolea Nabii kutokana nao, na ilhali Mwenyezi Mungu alimpa Ibrahim na ukoo wake - naye ni baba yenu (Mayahudi na Wakristo), na baba yao (Waislamu pia) - Kitabu kilicho teremshwa kwa ufunuo, na Unabii na Utawala ulio mkubwa!
Miongoni mwa walio pelekewa Nabii Ibrahim na ukoo wake wapo wenye kukiamini Kitabu kilicho teremshiwa kwao, na wapo walio kipa nyongo wakajitenga nacho. Na jaza ya hawa wenye kujitenga na wito wa Haki ni Jahannamu yenye moto wa kuteketeza.
Hakika wanao pinga hoja zetu zenye kubainisha wazi wazi, na wakawakanusha Manabii, tutakuja watia kwenye Moto utakao babua ngozi zao. Na kila zikisita kuhisi adhabu Mwenyezi Mungu atawabadilishia ngozi nyengine mpya ili machungu ya adhabu yabaki yakiendelea. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye ushindi katika mambo yake, na Mwenye hikima katika vitendo vyake. Humuadhibu mwenye kumpinga na akabaki na upinzani mpaka kufa kwake. Qur'an Tukufu imeitangulia sayansi ya kisasa, ikathibitisha kuwa katika ngozi mishipa ya kuhisi, Navo, imetanda kama wavu, na hiyo hupokea mishipa yote ya kuhisi machungu, joto na baridi na mengineyo. Na hayo hayakujuulikana ila hivi karibuni.
Na ambao walio yasadiki yaliyo wajia kutoka kwa Mola wao Mlezi, na wakatenda vitendo vyema, tutawalipa kwa Imani yao na vitendo vyao na tutawaingiza katika Mabustani ya Peponi yapitayo mito chini ya miti yake. Uhai wao hauna kikomo kabisa. Nao humo watakuwa na wake walio t'ahirika na kila la aibu na uchafu. Tutawapa uhai wa starehe chini ya vivuli vizuri vya kudumu, waishi maisha mema yenye neema isiyo kwisha.
Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni nyinyi Waumini mrejeshe vyote mlio pewa amana, kutokana na Mwenyezi Mungu au kutokana na watu, kwa wenyewe kwa uadilifu. Basi msifanye jeuri katika kuhukumu. Haya ni mawaidha yanayo toka kwa Mola wenu Mlezi. Basi yafanyieni pupa kuyafuata. Bora ya mawaidha ni yanayo tokana naye Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu daima ni Mwenye kusikia yasemwayo, ni Mwenye kuyaona yatendwayo. Basi anamjua anaye rejesha amana, na anaye fanya khiana, na anaye hukumu kwa uadilifu, na anaye fanya jeuri. Na kila mmoja atamlipa kwa atendalo.
Enyi mlio sadiki aliyo kuja nayo Muhammad! Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume, na wale wanao tawala mambo yenu miongoni mwa Waislamu wanao simama juu ya haki na uadilifu, na wanatekeleza Sharia ya Mwenyezi Mungu. Na mkizozana katika jambo baina yenu basi rejeeni kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake ili mpate kujua hukumu yake. Kwani Yeye Mwenyezi Mungu amekuteremshieni Kitabu chake na Mtume wake amebainisha hicho Kitabu. Na katika hayo ipo hukumu ya hayo mnayo khitalifiana kwayo. Haya ni kwa mujibu wa Imani yenu kumuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na haya ndio bora kwenu ili mpate kuongoka kwendea uadilifu katika mnayo khitalifiana kwayo, na mwisho wake ndio mzuri zaidi. Kwani hivyo ndio kuzuia zisitokee khilafu zinazo pelekea ugomvi na upotovu.