Na tutazitoa chuki zote ziliomo katika nyoyo zao. Basi watakuwa katika Janna, Pepo, ndugu wenye kupendana, ikipita mito ya maji matamu mbele yao. Watasema kufurahia neema watayo ipata: Alhamdulillahi, yaani Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu, ambaye aliye tuonyesha Njia ya kufikia neema hizi, na akatuwezesha kuifuata. Na ingeli kuwa hakutuhidi, kutuongoa, Mwenyezi Mungu kwa kutupelekea Mitume na akatupa tawfiq, tusingeweza sisi wenyewe kufikia uwongofu. Hakika Mitume wa Mola wetu Mlezi wametujia na wahyi wa Haki! Hapo tena Mwenyezi Mungu atawaambia: Hakika hii Pepo ni zawadi mmepewa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mmepewa kwa fadhila yangu bila ya kuwa nyinyi kutoa kitu, kama urithi. Na takrima hii mlio pata ni sababu ya vitendo vyenu vyema duniani.