Hatukuziumba mbingu na ardhi na vyote vilio baina yake ila kufuatana na sharia zilizo thibiti, kwa makusudio yanayo ambatana na hikima, na kwa muda maalumu ambao baada yake utakwisha. Na wale wanao ukataa ukweli huu wanapuuza yale waliyo onywa kwayo, ya kuumbwa kupya siku watakapo fufuliwa watu kwa ajili ya malipo.
Waambie hao wanao muomba asiye kuwa Mwenyezi Mungu: Hebu nambieni hali ya hao mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu. Nijuvyeni wameumba nini katika ardhi, au wana ushirika wowote katika mbingu? Nileteeni Kitabu kitokacho kwa Mwenyezi Mungu, au mabaki yoyote kutokana na ilimu za watu wa zamani ambayo mnayategemea kwa madai yenu, ikiwa mnasema kweli.
Na nani aliye zidi kupotea kuliko anaye muacha Mwenyezi Mungu akaiomba miungu mingine ambayo haitamjibu kitu mpaka mwisho wa dunia, na ambao hao hata hawana khabari ya maombi yao.