Walio takabari na wakajiona ni wakubwa, watawaambia wanyonge, kwa kuyapinga maneno yao: Kwani sisi tulikuzuieni msiongoke ulipo kufikieni uwongofu? Tumekuzuieni sisi au nyinyi wenyewe ndio mmekhiari upotofu kuliko uwongofu.
Na wanyonge nao watawaambia walio takabari: Bali vitimbi vyenu na uchochezi wenu kutuchochea usiku na mchana ndio umetutumbukiza katika hilaki, pale mlipo kuwa mkitutaka tumkufuru Mwenyezi Mungu, na tumfanyie miungu mingine ya kumshirikisha. Na pande zote mbili zikaficha majuto yao walipo iona adhabu inawashukia. Wakajua kuwa hapana faida ya kuonyesha majuto. Na tukayaweka makongwa, (nira), juu ya shingo za wasio amini. Je! Watu hawa wanastahiki chochote ila malipo kwa yale waliyo kuwa wakiyatenda?
Na sisi hatukumtuma Mtume yeyote kwenda kwenye mji kuwaita watu wake wafuate Haki ila wale wanao jidekeza kwa starehe zao katika ule mji husema: Hakika sisi tunayakanusha hayo mliyo kuja nayo.
Ewe Nabii! Waambie: Hakika aliye niumba humkunjulia riziki amtakaye, katika wanao muasi na wanao mt'ii. Na humdhikisha amtakaye. Wala hiyo si dalili ya kuwa Yeye yuradhi na mtu au anamchukia. Lakini watu wengi hawajui haya.
Wala mali yenu wala watoto wenu sio jambo la kukurubisheni kwetu mkawa karibu. Lakini ambaye Imani yake imethibiti, na akawa anatenda mema, basi watu kama hao ndio watapata thawabu mara mbili kwa waliyo yatenda. Na Peponi watakuwa ni watu wa juu na wenye amani.
Na hao ambao wana fanya juhudi kuzipinga Ishara zetu, wakifanya kila hila kuzivunja na kuwazuia Manabii wetu wasifikishe Ujumbe wake, hao, basi watakuwa katika adhabu, wamehudhurishwa na wala hawataepuka.
Ewe Nabii! Sema: Hakika Mola wangu Mlezi anamkunjulia riziki amtakaye katika waja wake, na humdhikisha amtakaye. Na chochote mtacho kitoa Yeye atakilipa. Na Yeye Aliye takasika ni Mbora wa wenye kuruzuku.