Ninaapa: Hakika katika watu wa Sabaa katika makaazi yao ya Yaman palikuwa na Ishara ya uweza wetu. Zilikuwako bustani mbili zilizo zunguka nchi yao, kulia na kushoto. Wakaambiwa: Kuleni katika riziki ya Mola wenu Mlezi, na mshukuru neema zake kwa kuzitumilia inavyo faa. Huu mji wenu ni mji mzuri, una vivuli na matunda. Na Mola wenu Mlezi ni Mwingi wa maghfira kwa anaye mshukuru.
Lakini wao waliacha kushukuru neema, na wakawa maisha yao ya kiburi. Tukawafungulia mafuriko ya nguvu yaliyo tokea baada ya kupasuka kuta za mahodhi, yakateketeza mabustani yao. Tukawabadilishia badala ya bustani zao mbili zile zenye matunda mazuri, zikawa nyengine mbili zenye matunda machungu, na miti isiyo kuwa na matunda, na mikunazi kidogo isiyo toa hamu. Hili liitwalo "Hodhi" la maji ya mvua kubwa au "Hodhi la Ma`arib" ni kubwa kuliko mahodhi yote ya Yaman. Hodhi hili linaweza kubadilisha ardhi kavu ya kiasi ya maili 300 ya mraba ikawa yenye rutba na mashamba. Na dalili ya hayo ni hizo bustani mbili zilizo tajwa. Wanazuoni wa taarikh (historia) wanakhitalifiana katika ujenzi wa hilo hodhi kuu. Vile vile zipo kauli mbali mbali kukhusu kubomoka kwake.
Hayo ndiyo malipo tuliyo walipa kwa kufuru zao kuzikufuru neema na kuto zishukuru. Na kwani Sisi tunamuadhibu kwa adhabu hii kali yeyote yule ila aliye kuwa mwingi wa kumkufuru Mwenyezi Mungu na fadhila zake?
Na tulifanya baina ya maskani yao ya Yaman na baina ya miji mingine iliyo barikiwa miji mingineyo pia iliyo karibiana inaonana. Na tukafanya makhusiano baina yao ni kiasi maalumu cha mwendo usio kuwa wa taabu. Na tukawaambia: Nendeni humo usiku na mchana nanyi mko katika amani.
Kwa kutakabari kwa neema, na raha, na amani, walisema: Tuwekee mbali masafa ya safari zetu, tusisadifu kukuta miji iliyo amirishwa ya katikati mpaka tufike huko twendako! Mwenyezi Mungu akazifanya ziwe mbali hizo safari zao. Na wakawa wao wamejidhulumu nafsi zao kwa uasi wao. Tukawafanya hao ni masimulizi ya watu, na tukawatenganisha mtengano mkubwa. Hakika katika yaliyo wapata hao yapo mawaidha kwa kila mwenye kusubiri kwa balaa, mwenye kushukuru kwa apewacho.
Na bila ya shaka Iblisi amehakikisha dhana yake juu yao. Nao wakamfuata yeye isipo kuwa wachache miongoni mwa Waumini.
Na wala Iblisi hakuwa na nguvu za kuwafanya wamt'ii na kumnyenyekea; lakini Mwenyezi Mungu kawafanyia mtihani apate kuwadhihirisha wepi wanao isadiki Akhera, na wepi wana shaka nayo. Ewe Nabii! Mola wako Mlezi ni Mwenye kuchungua kila kitu, Mwenye kusimamia kila kitu.
Ewe Nabii! Waambie washirikina: Waombeni hao mnao dai kwa uwongo kwamba ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu, wakuleteeni manufaa au wakuondoleeni madhara. Hawakujibuni kitu. Kwani hao hawamiliki hata kiasi ya chembe ya kitu katika mbingu wala katika ardhi. Wala wao hawana ushirika wowote na Mwenyezi Mungu katika kuumba au kumiliki. Wala hapana yeyote katika hao miungu ya uwongo anaye msaidia Mwenyezi Mungu katika kupanga mambo ya viumbe vyake.