Na hebu kumbukeni, enyi Waumini, katika hali ya kuwa mna nguvu, pale mlipo kuwa wachache na wanyonge. Maadui walikudhilini kwa unyonge wenu, nanyi mlishikwa na khofu wasije maadui zenu kukunyakueni. Basi tena mkahama kwa amri ya Mwenyezi Mungu, na makaazi yenu yakawa Yathrib (Madina). Na mkapata manusura kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na tawfiki yake, na akakuruzukuni ngawira njema kutaraji mtashukuru kwa neema hii, na muendelee katika Njia ya Jihadi kulinyanyua Neno la Haki.
Enyi mlio isadiki Haki mkaifuata! Haikufaliini kumkhini Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa kufanya urafiki na maadui wa Haki, na kukhuni katika ngawira, au kwa kuacha kwenda kwenye Jihadi. Wala msikhuni amana mnazo pewa nanyi mnajua amri na makatazo yake.
Enyi Waumini, wenye kusadiki! Jueni kuwa fitna ya nafsi zenu inatokana na kupita mpaka katika mapenzi yenu kwa watoto wenu na mali yenu. Basi isiwe kupenda kwenu kuyapenda mali na wenenu yakazidi kuliko mapenzi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hayo yatakuharibieni mambo yenu. Na jueni kuwa malipo ya Mwenyezi Mungu yanakutosheni kuliko mali na watoto.
Enyi mlio isadiki Haki na mkaifuata! Mkizinyenyekea amri za Mwenyezi Mungu kwa siri na dhaahiri, Mwenyezi Mungu atakujaalieni katika nafsi zenu uwezo wa kupambanua baina ya Haki na upotovu, na atakutunukieni ushindi wa kutenga baina yenu na maadui zenu, na atakusitirieni maovu yenu yaondoke, naye akusameheni. Na Yeye Subhanahu daima ni Mwenye fadhila kubwa.
Na kumbuka ewe Nabii, neema za Mwenyezi Mungu zilio juu yako, pale washirikina walipo panga njama kukutia nguvuni - ama wakufunge, au wakuuwe, au wakutoe mji! Hakika walikupangia mipango miovu! Na Mwenyezi Mungu Mtukufu alikupangia utokane na shari yao. Na mpango wa Mwenyezi Mungu ndio wa kheri, na una nguvu zaidi, na ndio wenye kushinda.
Na ewe Nabii! Kumbuka inda ya washirikina ulipo kuwa ukiwasomea Aya za Qur'ani Tukufu, nazo ni Ishara zetu. Ujahili wao na ghururi yao iliyo pita kiasi iliwapelekea kusema: Tungeli taka kusema kama isemavyo hii Qur'ani tungeli sema; kwani humu hamna chochote ila visa walivyo viandika watu wa kale!
Na kumbuka, ewe Nabii, vipi walivyo kuwa wanakupinga na kumpinga Mwenyezi Mungu hata kwa inda yao wakasema kumwambia Mwenyezi Mungu, Mola wao Mlezi: Ikiwa haya unayo kuja nayo ni mambo madhbuti, basi zijaalie mbingu zitunyeshee mawe, au tuletee adhabu yoyote iliyo kali yenye uchungu!
Si katika hikima ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwaadhibu katika dunia kwa adhabu kali na hali wewe upo miongoni mwao unaitia Haki, nawe unataraji asaa wataitikia. Wala si mtindo wa Mwenyezi Mungu kuwaadhibu wenye kuasi nao wangali wanamuomba maghfira na wamo kuyavua yale waliyo nayo.