Watasema nao wanakiri makosa yao : Ewe Mola wetu Mlezi! Maasi yetu yalikuwa mengi, ndio yakatupatia mashaka, na tukawa wenye kupotea tukaiacha njia ya sawa.
Na watasema: Mola wetu Mlezi! Tutoe Motoni na uturejeshe duniani. Basi tukirudi tena kwenye ukafiri na uasi basi tutakuwa kweli ni twenye kujidhulumu nafsi zetu.
Mimi sikukudhulumuni, bali nyinyi mmejidhulumu wenyewe. Kwani Waumini wema katika waja wangu walikuwa wakisema duniani: Ewe Mola wetu Mlezi! Tumeamini. Basi tughufirie na uturehemu. Na Wewe ndiwe Mbora wa wanao rehemu.
Na nyinyi daima mlikuwa mkiwafanyia maskhara, mpaka maskhara yenu yakakusahaulisheni kunikumbuka Mimi na kuniabudu Mimi. Basi hamkuamini wala hamkut'ii. Nanyi mlikuwa mkiwacheka kwa kejeli.
Watasema kwa kuyaona mafupi maisha yao kwa adhabu wanayo ikuta: Tuliishi muda wa siku moja au baadhi ya siku hivi. Basi waulize wanao weza kuhisabu, sisi tumeshughulishwa na hii adhabu.
Basi Mwenyezi Mungu atawaambia: Hamkuishi duniani ila muda mchache tu. Na lau ingeli kuwa mnajua malipo ya ukafiri na uasi na kwamba starehe ya duniani ni chache mngeli amini na mkat'ii.
Je? Mlidhani kuwa tuliwaumbeni bila ya hikma, ndio mukafanya ufisadi katika ardhi, na mkadhani kuwa hamtafufuliwa mpate kulipwa.
Utukufu ni wa Mwenyezi Mungu peke yake. Na Yeye ndiye Mwenye kumiliki ufalme wote. Hapana Mwenye kuabudiwa kwa Haki isipo kuwa Yeye. Na Yeye ndiye Mwenye A'rshi Tukufu.
Na mwenye kumuabudu mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu hana ushahidi wa kumfanya huyo astahiki kuabudiwa. Hakika Mwenyezi Mungu atampa adhabu kwa ushirikina wake bila ya shaka yoyote. Hakika makafiri hawaongokewi. Bali watao ongokewa ni Waumini.
Na sema, ewe Nabii, ukimlingania Mwenyezi Mungu na kumnyenyekea: Ewe Mola wangu Mlezi! Nisamehe dhambi zangu, na nirehemu. Kwani Wewe ni Mbora wa wanao rehemu, kwa sababu rehema yako imeenea na ipo karibu kwa watendao mema.