Na hakukuwa kuichelewesha miezi mitakatifu, au baadhi yake, kuliko alivyo iweka Mwenyezi Mungu, ila ni kuzidi ukafiri, kama walivyo kuwa wakifanya watu wa kijahiliya. Hao makafiri wakizidisha hivyo kuongeza upotovu juu ya upotovu! Waarabu wakati wa ujuhali walikuwa hufanya mwezi uliyo harimishwa kupigana vita kuwa ni wa halali, pindi wakihitajia kupigana. Na hufanya mwezi ulio halalishwa ndio ulio harimishwa. Na wakisema: Mwezi kwa mwezi. Yaani kulipizia ipate kutimia idadi ile aliyo harimisha Mwenyezi Mungu. Matamanio yao yamewapendezeshea kitendo chao hicho kiovu. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu walio shikilia kukataa kuifuata Njia ya kwendea Kheri.
Enyi Waumini! Mna nini, anapo kwambieni Mtume: Tokeni mwende kwenye Jihadi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu baadhi yenu mkafanya uzito kutoka? Haikufalieni hivyo! Mnaona afadhali maisha ya dunia yatayo kwisha, kuliko maisha ya Akhera na neema zake za kudumu? Starehe ya duniani na utamu wake ukilinganisha na starehe ya Akhera ni chache na upuuzi.
Msipo muitikia Mtume, mkatoka nje kwenda pigana Jihadi, Mwenyezi Mungu atakupeni adhabu iliyo chungu, na Mola wenu Mlezi atawabadilisha watu waje wengine, sio nyinyi, wamuitikie Mtume wala hawatobaki nyuma ikinadiwa Jihadi. Wala nyinyi kwa kukataa kwenu kwenda pigana, hamtamdhuru Mwenyezi Mungu chochote. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uwezo mkubwa juu ya kila kitu.
Enyi Waumini! Ikiwa nyinyi hamtasaidia kumnusuru Mtume wa Mwenyezi Mungu, basi. Kwani Mwenyezi Mungu anatosha Yeye kumnusuru. Kama pale alipo msaidia na akamnusuru alipo tolewa Makka kwa kahari na makafiri, naye hana mwenziwe ila Abu Bakar peke yake. Wakawa wao wawili pangoni wanajificha wasionekane na washirikina walio kuwa wanawasaka wawaadhibu na kuwauwa. Abu Bakar akawa anamkhofia Mtume maisha yake. Mtume akamwambia kumpoza: Usihuzunike! Kwani hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi, kwa kutunusuru na kutusaidia. Hapo Mwenyezi Mungu akamteremshia Abu Bakar utulivu, na akamuunga mkono Mtume kwa askari walio toka kwake, na ambao hawawajui ila Yeye Subhanahu. Na mambo yakamalizikia kuwa shari ya washirikina ikavia na Dini ya Mwenyezi Mungu ikashinda. Na Mwenyezi Mungu anasifika kuwa ni Mwenye nguvu, hashindiki, ni Mwenye hikima hapotei katika mipango yake. Hilo pango alilo jificha Nabii s.a.w. na rafiki yake Abu Bakar r.a. lilikuwa katika mlima wa Thor, karibu na Makka. Wakakaa humo siku tatu, baadae wakatoka usiku walipoona msako umetulia. Walifika Madina taarikh 8 katika Mwezi Rabii'ul awwal (Mfungo Sita) mwaka wa kwanza wa Hijra. (20 Septemba, 630 kwa taarikh za Kizungu.)