Ewe Nabii! Shikamana na juhudi ya kuwazuia makafiri na ukafiri wao, na wanaafiki na unaafiki wao. Na wakazanie katika juhudi yako. Makaazi yao hawa aliyo waahidi Mwenyezi Mungu huko Akhera ni Jahannamu. Na uovu ulioje mwisho huo!
Hao wanaafiki wanaapa mbele yako, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwamba hawakusema jambo baya katika hayo uliyo ambiwa. Nao ni waongo katika kukataa kwao, wanaapa kiapo cha uwongo! Na wao hakika wamesema neno la kufuru. Na ukafiri wao sasa umebainika, baada ya kuwa kwanza umefichika. Na hapana sababu yoyote ya kukuchukia ila ni kiburi kwa neema walizo pewa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kwa kule kupewa ngawira walizo shirikiana na Waislamu! Wakirejea kwa Mwenyezi Mungu, wakaacha unaafiki wao, na wakajuta kwa waliyo yatenda, toba yao itakubaliwa. Na hivyo itakuwa kheri kwao. Wakiitupa Imani, basi Mwenyezi Mungu atawaadhibu duniani kwa namna mbali mbali za balaa, na kesho Akhera atawatia katika Moto wa Jahannamu. Wala hawatapata katika ardhi wa kuwapigania, au wa kuwaombea, au wa kuwanusuru.
Katika wanaafiki wapo ambao humuapia na kumuahidi Mwenyezi Mungu kuwa akiwapa mali na akawatajirisha kwa fadhila yake, basi watatoa sadaka na watakuwa wenye vitendo vyema.
Mwenyezi Mungu akiwaitikia na akawapa kwa fadhila yake, wanafanya ubakhili. Hawatoi kitu, wala hawatimizi ahadi, na huiacha kheri wakiipuuza na wakimpuuza Mwenyezi Mungu.
Matokeo ya ubakhili wao ni kujaa unaafiki katika nyoyo zao mpaka watakapo kufa na wakakutana na Mwenyezi Mungu, kwa sababu ya kuvunja ahadi zao na uwongo wao katika viapo vyao.
Vipi wanajitia ujinga na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwajua vyema? Hapana chochote wanacho dhamiria kisirisiri katika kuvunja ahadi kinacho fichikana kwake. Wala wanacho kinong'ona kwa uficho katika kuitia kombo Dini na kuwapangia njama Waislamu. Naye, aliye tukuka shani yake, ni Mjuzi mno hapitikiwi na kitu chochote..
Na katika ila zao hawa wanaafiki pamoja na ubakhili wao ni kuwa wao huwakejeli Waumini wenye nafasi kwa vile kusabilia mali yao kwa wanao hitajia, na huwafanyia maskhara wale wenye nafasi ndogo wanao toa sadaka juu ya kuwa wenyewe walicho nacho ni kidogo. Mwenyezi Mungu kesha walipa kwa hizo kejeli zao kwa kuwakashifu wakatambulikana fedheha zao, wakawa wao ndio kichekesho cha watu wote. Na kesho Akhera adhabu yao itakuwa kali.