Nuun, ndio harufi ya N, iliyo anzia Sura hii ni kama kupinzana na hao wanao kadhibisha, na ili kuwazindua wenye kusadiki. Naapa kwa kalamu wanayo andikia Malaika na wenginewe, na hayo mambo ya kheri na manufaa wanayo yaandika,
Hakika Mola wako Mlezi, Yeye ndiye Mwenye kumjua zaidi aliye iacha Njia yake, na Yeye ndiye Mwenye kuwajua zaidi wenye akili walio ongoka kumwendea Yeye.
Wanatamani lau ungeli kuwa laini kwao katika baadhi ya mambo, ili na wao wawe laini kwako, kwa tamaa upate kurudishiana nao. (Neno lililo tumiwa hapo "Tud- hinu fayud-hinuun", maana yake khasa "Upake mafuta na wao wapake mafuta". Kiswahili husema: Kumpaka mtu mafuta kwa mgongo wa chupa. Yaani kumpa sifa za uwongo, kumfanyia unaafiki. Kwa Kiarabu ni "Mudaahana". Kupakana mafuta)
Sisi tumewafanyia mtihani watu wa Makka kwa kuwapa neema, nao wakazikufuru; kama tulivyo wafanyia mtihani hao watu wenye shamba, walipo chukua kiapo kuwa watakwenda vuna mazao ya shamba lao asubuhi mapema,
Alisema aliye kuwa muadilifu wao na mbora wao akiwalaumu: Sikukwambieni mlipo kuwa mnasemezana kuwanyima masikini, hebu hamumkumbuki Mwenyezi Mungu mkaiacha niya yenu?
Wakasema walipo rejea kwenye uwongozi wao: Tunamtakasa Mwenyezi Mungu kuwa katudhulumu kwa yaliyo tusibu. Hakika sisi wenyewe ndio tumejidhulumu kwa makusudio yetu maovu.
Asaa Mola wetu Mlezi akatupa badala lilio bora kuliko hili shamba letu. Hakika sisi tunamtaka Mola wetu Mlezi peke yake atupe msamaha na malipo.
Mfano wa kama hayo yaliyo yasibu hilo shamba ndio inakuwa adhabu yangu ninayo iteremsha duniani kwa anaye stahiki. Na bila ya shaka adhabu ya Akhera ni kubwa zaidi lau kuwa watu wanajua hayo.
Au kwani mnazo ahadi juu yetu zenye kutiliwa mkazo kwa viapo, zenye kubaki mpaka Siku ya Kiyama, kwamba mnayo haki ya hayo mnayo jihukumia?
Kwani wanao wanao shirikiana nao, na wanao fuata mwendo wao katika kauli yao hii? Basi na wawalete hao washirika wao, ikiwa wao ni wasema kweli katika madai yao.
Siku mambo yatapo shitadi na yakawa magumu, na wakatakiwa makafiri wasujudu kwa kuwaemea na kuwakejeli, na wasiweze, (Kuwekwa wazi mundi, ni kinaya ya kudhihirishwa kweli yote Siku ya kwima kondo, Siku ya Kiyama. Chambilecho Sayyid Abdulla bin Ali bin Nassir katika Al Inkishaf: Tafakari siku ya kwima kondo Ya kuaridhiwa kila kitendo Pindi madhulumu atapo ondo Achamba Ya Rabi namua naye)
Macho yao yameinama chini, yamefunikwa na fedheha. Na duniani walikuwa wakitakiwa wasujudu walipo kuwa wakiweza na wakakataa kusujudu.
Ewe Muhammad! Nachilie na hao wanao ikadhibisha Qur'ani. Tutawajongeza kwenye adhabu kidogo kidogo kwa jiha wasio ijua kuwa adhabu itatokea huko.
Basi wewe subiri kwa tunavyo wapa muhula na kukuakhirisha kukuletea manusura yetu juu yao. Wala usiwe kama Yunus, aliye mezwa na samaki, akawa na haraka na kuwaghadhibikia watu wake, alipo mnadia Mola wake Mlezi, naye kajaa hasira na ghadhabu, akitaka waadhibiwe kwa haraka.
Lau kuwa neema ya Mola wake Mlezi haikumdiriki kwa kukubali toba yake, angeli tupwa kutokana na tumbo la samaki ufukweni, naye akiteseka kwa kuteleza kwake.
Na makafiri wangeli karibia kukutelezesha na pahala pako, kwa jicho lao wanalo kuangalia kwa uadui na chuki wanapo isikia Qur'ani, wakisema: Hakika huyu ni mwendawazimu.