Na hakika hii Qur'ani iliyo thibiti katika Lauhun Mahfuudh, Ubao ulio hifadhiwa, ulioko kwetu, bila ya shaka, ina cheo cha juu, na imepangwa kwa mpango wa hikima, katika mwisho wa ufasihi. (Vitabu vyote vya mbinguni asili yake anayo Mwenyezi Mungu, katika Ujuzi wake wa tokea azali, Al- I'lmu al-azaliy au Ubao Ulio Hifadhiwa Al-lauhu al-mahfuudh au Asili ya Maandiko Ummu-l-kitabi. Kwa sababu ya kuwa Vitabu vilivyo kuja zamani, ikiwa Taurati, Zaburi, Injili n.k. vilikuwa ni vya muda fulani, na kwa mataifa fulani, basi haikuwepo dharura vibaki kwa usafi kila neno lake. Ni makusudio yake tu yabakie, yaliyo kuwa ya msingi. Ama ulipo fika wakati wa kudumisha Ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa zama zote, na kwa watu wote, ndio ikaja Qur'ani ambayo imehifadhiwa kila neno lake. Na ndio siri ya kuletwa kwa lugha ya Kiarabu na ikalindwa kwa lugha ile, ijapo kuwa itatarajumiwa katika lugha nyengine. Mzozano wowote unao tokea unarejezwa kwenye asli ile ya Kiarabu ambayo haikubadilika hata chembe, wala haitabadilika mpaka Siku ya Kiyama. Huo peke yake ni muujiza. Ama vitabu vya Biblia ni kama maji yaliyo tibuliwa na ng'ombe mpaka kwenye chemchem yake. Chemchem ya Qur'ani haikutibuliwa. Ijapo kuwa wanyama na watu wanaweza kunywa maji yake huku chini, kwenye kitovu cha chemchem hakuguswi. Huko ni kwenye Qur'ani hiyo ya Kiarabu, safi kama ilivyo kwenye Ubao Ulio Hifadhiwa.)
Je! Tukupeni muhula, tuache kukuteremshieni Qur'ani kwa kukutupilieni mbali, kwa sababu ya kupita kwenu mipaka ya ukafiri juu ya nafsi zenu? Hayawi hayo, kwa kufuata hukumu ya kulazimikana kwenu na hoja.
Basi tuliwateketeza walio kadhibisha walio tangulia; na hao walikuwa wamewazidi makafiri wa Makka kwa nguvu na ushupavu. Basi wasidanganyike hawa na ujabari wao. Na zilikwisha tangulia katika Qur'ani hadithi za ajabu za watu wa kale, za kuwafanya wenginewe wazingatie. Basi enyi mnao kanusha! Zingatieni!
Na ninaapa, ewe Mtume! Ukiwauliza makafiri nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema kuyajibu hayo: Mwenyezi Mungu ndiye aliye ziumba, ambaye anasifika kwa hakika ya mambo kuwa ni Mwenye nguvu, na Mwenye Ujuzi ulio enea.
Ambaye amekufanyieni ardhi ni pahala palipo tanda, ili muweze kukaa humo na mjitumilie, na akakufanyieni ndani yake njia mnazo zipitia katika safari zenu mpate kufikia mtakako.