Na wale wanawake wanao zini wakishuhudiwa na mashahidi wanaume wane walio waadilifu, basi wazuieni wasitoke nyumbani kwa ajili ya kuwalinda na kuzuia usiendelee ufisadi na shari mpaka wafe, au Mwenyezi Mungu awafungulie njia ya maisha yaliyo sawa kwa kuolewa na kutubu. (Wafasiri wengine wanasema hukumu hii ni kwa wanawake wanao fanya mambo machafu wenyewe kwa wenyewe, sio ya zina baina ya mwanamke na mwanamume. Kwa kuhifadhi heshima ya wanawake inalazimu wapatikane mashahidi wane, badala ya wawili, walio ona kitendo khasa, sio kuwatuhumu watu kwa jambo ovu kama hilo bila ya mashahidi wane walio shuhudia kwa macho yao.)
Mwanamume na mwanamke walio zini, nao hawajaoa (au kuolewa), wapewe adhabu maalumu, pindi ikithibiti hiyo zina kwa mashahidi wane waadilifu. Wakitubu baada ya kupewa adhabu, basi msiwatajie hayo maasi waliyo yatenda, wala msiwaaziri. Hakika Mwenyezi Mungu kwa rehema yake anakubali toba ya wenye kutubu.
Hakika toba imedhaminiwa na Mwenyezi Mungu kwa watendao maovu katika hali ya ujinga, na kupitikiwa na kutoangalia vyema, kisha wakafanya haraka ya kutubu kabla ya kufikiwa na mauti. Hawa basi Mwenyezi Mungu anaikubali toba yao, naye ni Mjuzi, haumfichikii ukweli wa toba, ni Mwenye hikima, hakosei katika kupima.
Toba isiyo kubaliwa ni ya wanao fanya maasi kisha hawafanyi haraka kuyajutia mpaka mmoja afikwapo na mauti. Tena hapo husema: Sasa mimi natangaza majuto na toba. Kadhaalika toba haikubaliwi kutokana na wanao kufa katika ukafiri. Mwenyezi Mungu ameyaandalia makundi mawili hayo adhabu ya kutia uchungu huko kwenye nyumba ya malipo, Akhera.
Enyi mlio amini! Haikujuziini kuwafanya wanawake kama bidhaa, mkiwarithi wake zenu bila ya mahari na bila ya ridhaa yao. Wala msiwadhulumu kwa kuwadhikisha ili wapate kusamehe baadhi ya mahari mlio wapa. Wala msiwadhiki ili wapate kukurejesheeni mali mlio wapa, ila ikiwa wakifanya kosa wazi la kuwacha ut'iifu, au la tabia mbovu, au la ukahaba. Hapo mnaweza kuwadhikisha au kuchukua baadhi ya mlicho wapa wakati wa kufarikiana nao. Na ni waajibu wenu, enyi Waumini, kukaa na wake zenu kwa vizuri, kwa maneno mema na vitendo vyema. Ikiwa mtawachukia kwa aibu fulani katika tabia au katika umbo au mengineyo, basi juu ya hivyo subirini. Msifanye haraka kuwaacha, kwani asaa Mwenyezi Mungu akajaalia kheri nyingi katika hicho hicho mkichukiacho. Na ujuzi wa mambo yote uko kwa Mwenyezi Mungu tu.