Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na kutokana na nafsi hiyo akamuumba mkewe, na kutokana na hao wawili, wakaenea wanaume na wanawake wengi. Basi nyote mnatokana na nafsi moja. Mcheni Mwenyezi Mungu mnaye mtaka msaada kwa kila mnacho kihitajia, na kwa jina lake ndio mnaombana nyinyi kwa nyinyi katika mambo yenu. Pia tahadharini na kuacha kuwasaidia jamaa zenu, wa karibu na wa mbali. Kwani Mwenyezi Mungu daima anakuangalieni. Hapana chochote katika mambo yenu kinacho fichikana kwake. Na Yeye ndiye Mwenye kukulipeni.
Na wapeni mayatima mali yao wanayo stahiki, na yalindeni mali yao vizuri, wala msiwape kilio duni mkawanyima kizuri. Wala msichukue mali yao mkaongezea kwenye mali yenu. Hakika kitendo hicho ni dhambi kubwa.
Ilivyo kuwa mnakhofu kuwadhulumu mayatima kwa kuwa hiyo ni dhambi kubwa, basi kadhaalika khofuni machungu ya wake zenu kwa kuacha kuwafanyia uadilifu baina yao, na kuzidisha juu ya wane. Basi mnaweza kuoa wawili, au watatu, au wane, ikiwa mna imani kuwa mtaweza kufanya uadilifu. Mkiogopa kuwa hamtaweza kufanya uadilifu basi oeni mmoja tu, au jitoshelezeni na wajakazi walio milikiwa na mikono yenu ya kulia. Hayo ni afadhali kuliko kwenda kuingia katika dhulma na ujeuri . Na ni afadhali msije mkawa na watoto wengi bila ya kiasi hata mshindwe kuwatazama. (Wafasiri wengi wamependelea kufasiri "Alla Tau'luu" kuwa "Kutofanya jeuri au dhulma." Lakini hii AL MUNTAKHAB imekhiari tafsiri hii ya "msikithirishe wana", ambayo ndiyo aliyo ifuata Imam Shaafii r.a., naye alitanguliwa na Maimamu wanazuoni wa Kiislamu, Zayd bin Aslam r.a.na Jabir bin Zayd r.a. kama alivyo simulia Daar Qut'ni, na imetajwa katika Tafsir ya Qurt'uby juzuu ya 5 sahifa 22.) Sharia ya Kiislamu si peke yake inayo ruhusu kuoa wake wengi, miongoni mwa sharia za dini za mbinguni. Sharia ya Taurati inamruhusu mwanamume kuoa idadi ya wanawake atakao. Na imetaja kuwa Manabii walikuwa wakioa wake kwa makumi na makumi. Na Taurati ni katika Agano la Kale la Biblia ambalo linafuatwa pia na Wakristo katika mambo ambayo hayakukatazwa katika Injili au Barua za Mitume. Na hakika iliopo ni kuwa hapana popote katika Agano Jipya panapo pinga sharia hiyo ya kuruhusu kuoa wake zaidi ya mmoja. Kanisa katika Karne za Kati liliruhusu hayo, na wafalme wa Ulaya wa Kikristo walio kuwa na wake wengi ni maarufu katika taarikh (historia). Khitilafu iliyopo ni kuwa Uislamu ndiyo dini ya kwanza kuweka idadi maalumu, isipindukiwe. Imeweka kiwango kwa mambo matatu. (Kwanza) wasipindukie hao wake kuliko wane. (Pili) asidhulumike mmoja katika hao wake, (Tatu) awe mtu anaweza kuwakimu hao wake. Shuruti mbili za mwisho zimelazimu kila ndoa, ijapokuwa ni ya kwanza. Wanazuoni wa Kiislamu wa sharia na wanga khitalifiana wanakubaliana pamoja kuwa mume ambaye anajua kuwa hawezi kuwafanyia uadilifu wakeze ni haramu kwake kidini kuongeza wake. Ila uharamu huu ni wa kidini, watawala na mahakimu hawawezi kumuingilia. Kwani uadilifu ni jambo la nafsi yake mtu, na dhamiri yake, na uwezo wa kutazama ni jambo la mnasaba halifungamani na mizani mojapo. Ni yeye mwenyewe atakaye pata adhabu Siku ya Kiyama akikhalifu amri hiyo. Dhulma au kutokuweza kukimu kunategemea hali ya siku zijazo, na mikataba haifungamani na mambo ambayo huenda yakawa au yasiwe, bali ni juu ya yaliyoko, na ilivyo kuwa dhaalimu huenda akawa muadilifu, na asiye weza sasa hueza akaweza baadae, kwani mali huja na kuondoka, juu ya hivyo Uislamu unasema mwanamume akimdhulumu mkewe au akashindwa kumkimu, basi mwanamke anaweza kutaka kufarikishwa na mume huyo, lakini hazuiliki na kuandikiana mkataba akifanya hayo kwa radhi yake na khiari yake. Na Uislamu kwa kufungua mlango wa kuoa wake zaidi ya mmoja lakini kwa mikazo kama hivyo ilivyo elezwa imekuwa umepiga vita magonjwa ya kijamii: Kwanza - Huenda ikawa idadi ya wanaume wanao faa kuoa ikawa chini kuliko wanawake wanao faa kuoelewa. Khasa huwa hayo baada ya vita. Imeonakana katika baadhi ya nchi za Ulaya imewahi kufika idadi ya wanawake kuwazidi wanaume baada ya vita kwa mara saba! Kwa hivyo ni hishima ya mwanamke katika hali kama hizo kuwa mke-mwenza kuliko kuwa akibahashika kama malaya, bila ya mume. Pili - Huenda kutokea baina ya mwanamume na mwanamke hali inayo walazimisha ama waingiane kiharamu au waoane kisharia. Ni maslaha kwa umma yawe hayo kwa mujibu wa sharia. Na ni bora kwa mwanamke kuwa mke kuliko kuwa hawara wa mwanamume huyu baada ya huyu. Ikiwa hii ni sura mbaya ya kuoa wake wengi, basi juu ya hivyo ni afadhali kuliko kuwa na mke mmoja. Kwani kuoa wake zaidi ya mmoja kama itavyo kuwa vibaya kunakinga shari kubwa zaidi kwa umma, nayo ni umalaya na maovu yanayo pandana nayo. Tatu - Mwanamke hakubali kuolewa na mume mwenye mke ila ikiwa ni kwa dharura iliyo kweli. Ikiwa mke wa kwanza atapata madhara kwa uke-wenza, basi huyu mwenzie atapata madhara makubwa zaidi kwa kuharimishwa mume kabisa, kwa kuwa ama ufe uke wake au apotee kwa wanaume majiani. Madhara makubwa hukingwa kwa madhara yaliyo akali (Kidogo). Nne - Imeonakana kuwa vijana wengi hawapendi kuoa, hata inakisiwa kuwa vijana wanao oa kwa kulinganisha na wafaao kuoa hawazidi kuliko 60%. Na haya yanazidi kila mwaka. Kupinga khatari hii hapana ila kuruhusu kuoa wake wengi. Tano - Huenda mke akapata maradhi ambayo hayamruhusu kulala na mumewe, au huenda akawa tasa. Ni maslaha ya umma na maslaha ya binafsi kuoa mke mwengine. (Wakati huo huo ikawa kumpa talaka huyo mke ni madhara makubwa zaidi kwa mke na ukatili kwa mume kufanya.) Kwa sababu kama hizi na nyenginezo Uislamu umeufungua mlango kwa shida na dhiki, na haukuufunga kabisa. Hivi sasa tunamwona Askofu Mkuu katika Uingereza anaona kuwa dawa ya pekee ya kuondoa uharibifu ulio uingilia ukoo wa Kiingereza ni kufungua mlango wa kuoa wake zaidi ya mmoja. Hakika Uislamu ni Sharia ya Mwenyezi Mungu ambaye anajua kila kitu. Kwani Yeye ndiye Mjuzi Mwenye hikima. (Haya tukijua kuwa dini ya Kikristo haikatazi kuoa wake wengi. Ni sharia zilizo tungwa na makanisa ya Kizungu tu kwa kufuata mila zao ndizo zinazo lazimisha kuoa mke mmoja. Basi hiyo ni mila ya Wazungu, wala si sharia ya dini yoyote duniani. Bali Uislamu ndiyo Dini pekee katika dini zote iliyo wekea kiwango, na kudhibiti idadi ya wanawake kuoa, kwa maslaha ya Umma.)
Wapeni wanawake mahari yao kuwa ni kipawa, tunza iliyo safi. Na nyinyi hamna haki yoyote katika hayo mahari. Ikiwa hao wanawake kwa radhi ya nafsi zao wenyewe wakakubali kusamehe sehemu yoyote ya mahari mliyo kwisha ahadiana, basi hapo mnayo ruhusa kuchukua na mkatumia kwa kheri na salama.
Wala msiwape wasio na akili ya kutosha kuendesha mambo yao mali yao, nayo ni mali yenu vile vile. Kwani mali ya yatima na ya mchache wa akili yamekulazimuni myatazame yasiharibike. Mwenyezi Mungu ameyajaalia mali hayo ya kukimu maisha. Wapeni kutokana na pato lake sehemu kama wanavyo hitajia kwa kula, na wavisheni na muwatendee vyema, na mseme nao maneno ya kuwaridhisha sio ya kuwaudhi au kuwadhili.
Na kabla ya hao mayatima kufika umri wa kubaalighi wajaribuni, mpate kujua akili zao na hali zao na maarifa yao katika kuendesha mambo. Hata wakifika wakati wa kusilihi kuoa na mkauona uwekevu wao, na matayarisho kuchukua jukumu, basi hapo wapeni mali yao wenyewe. Wala nyinyi msiyale mali yao kwa fujo, mkifanya haraka mpatilize kabla hawajabaalighi wakawa watu wazima ikabidi haki yao kurudi. Na akiwa katika mawasii anajitosha kwa utajiri, basi ajizuie asichukue chochote kuwa ni ujira kutazama mali ya mayatima. Na akiwa fakiri muhitaji basi ajitosheleze kuchukua ujira wa uangalizi kwa kadri ya ada ilivyo. Na mnapo wakabidhi mayatima mali yao wekeni mashahidi wa kushuhudia. Na mjue kuwa Mwenyezi Mungu daima yupo nyuma yenu, na Yeye ndiye Mhasibu, na Yeye ndiye Muangalizi. Na Yeye anatosha kuwa Mhasibu na Muangalizi.