Na kumbukeni katika neema zetu juu yenu kuwa tumekuokoeni kutokana na mateso ya Firauni na wasaidizi wake walio kuwa wakikuonjesheni adhabu kali kabisa, kwa kuwa wakiwachinja wana wenu wanaume - kwa khofu kuwa miongoni mwao atatokea wa kupindua utawala wa Firauni - na wakiwabakisha wanawake ili wawafanye wajakazi wao wa kuwatuma. Na katika adhabu hizi na uteketezaji huu wa umma ni majaribio makuu kutokana kwa Mola wenu, na ni mtihani mkuu kwenu.
Kumbukeni vile vile katika neema alizo kuneemesheni Mwenyezi Mungu pale tulipo kupasulieni bahari - na tukayagawa maji katikati ili mpate kupita - mkaokoka, Firauni na askari wake wasikupateni. Na kwa fadhila yetu mkavuka na tukawapatiliza adui zenu kwa sababu yenu, tukawazamisha mbele ya macho yenu. Nyinyi mkawa mnawaona wanazama, na bahari ikiwafunika baada ya nyinyi kwisha vuka salama.
Na kumbukeni wakati Mola wenu alipo agana na Musa muda wa masiku arubaini kwa ajili ya mazungumzo. Alipo kwenda walipo agana na akarejea alikukuteni mmekwisha geuka, na mkamfanya ndama aliye muunda Saamiriyu ndiye wa kuabudiwa. Mkawa kwa hivyo ni wenye kudhulumu kwa kumfanyia Mwenyezi Mungu aliye kuumbeni na kukuokoeni ana mshirika wake. ("Masiku" ni wingi wa Usiku. Wingi wa siku ni siku, kama ilivyo sahani, sabuni, silaha, sinia, sungura, saa. Ni makosa kwa Kiswahili kusema "masiku" kuwa ni wingi wa siku; "Masiku" ni wingi wa "Usiku". Kutumia "Masaa" kuwa ni wingi wa "Saa" ni makosa.)
Kisha tukakusameheni na tukaifuta adhabu yenu mlipo tubu na mkapata msamaha kwa dhambi zenu, ili mpate kumshukuru Mola Mlezi wenu kwa huko kufuta kwake makosa yenu, na kusamehe kwake, na fadhila zake.
Na kumbukeni tulipo kuneemesheni kwa kukumteremshia Nabii wenu Musa Kitabu chetu Taurati, Kitabu ambacho kinafarikisha baina ya Haki na baat'ili, na kinabainisha baina ya Halali na Haramu, ili mpate kupata uwongozi kwa nuru yake na muongoke kutokana na upotovu kwa kuzingatia yaliyomo ndani yake.
Ikumbukeni siku alipo kwambieni Mtume wenu Musa: Enyi watu wangu! Mmejidhulumu kwa kumchukua ndama wa Saamiriyu mkamuabudu. Basi tubuni kwa Mola wenu aliye kuumbeni kabla hamjawa kitu, kwa kuzighadhibikia nafsi zenu ovu zenye kuamrisha maovu, na zifanyeni hizo nafsi ziwe nyonge, ili mpate nafsi mpya zilio safi. Mwenyezi Mungu alikusaidieni kwa hayo na akakuwezesheni mkaweza, na hiyo ni kheri itokayo kwa Muumba wenu. Na haya ni kabla ya kutubu kwenu, Naye akakusameheni. Kwani Yeye ni mwingi wa kukubali toba kwa waja wake, na mwingi wa kuwarehemu.
Na kumbukeni kauli yenu mlio mwambia Musa: Kwamba sisi hatukukubali wewe mpaka tumwone Mwenyezi Mungu waziwazi hivi hivi kwa macho bila ya kificho. Ikakuchukueni radi na moto kutoka mbinguni, ikakutikiseni kuwa ni malipo ya inadi yenu na dhulma zenu, na kutaka kwenu jambo ambalo ni muhali kutokea kwenu. Nanyi mnaiona hali yenu na balaa na adhabu zilizo kusibuni kwa mpigo wa radi hiyo.
Kisha tukakuzindueni kutokana na huko kudawaa kwenu na kupwelewa, na tukakufundisheni ili mpate kuishukuru neema yetu kwa hayo, na mpate kuiunga mkono Haki ya Mwenyezi Mungu kwa kupitia njia ya shukrani hii.
Na katika fadhila zetu juu yenu ni kuwa tumekuleteeni mawingu yawe kama ni kivuli kukulindeni na mwako wa jua kali, na tukakuteremshieni Manna, nacho ni kitu kitamu kama asali kinaanguka juu ya miti linapo chomoza jua. Kadhaalika tumekuteremshieni Salwa, naye ni ndege aliye nona, nao wakikujieni kwa makundi asubuhi na jioni ili mle mstarehe. Na tukakwambieni: Kuleni vilivyo vyema katika riziki yetu. Hawa watu wakaikufuru neema. Na haya hayakutudhuru Sisi, lakini wamejidhulumu nafsi zao. Kwani madhara ya uasi unawarejea wao watendao. Katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na tukakuteremshieni Manna na Salwa" imetajwa kwa uhakika wa kisayansi, kwani hivi mwishoni imevumbuliwa kuwa madda za "Protein" zenye asli ya vinyama kama vile nyama na ndege ni bora kumfaa mtu kwa chakula kuliko "Protein" zinazotoka katika mimea na mboga. Na katika Manna mna sukari ya kumpa mtu nguvu na uchangamfu wa kufanyia kazi na kutaharaki huku na huku.