Mnapo wawacha wake wakakaribia kumaliza eda zao mnaweza kuwarejea kwa makusudio ya uadilifu na kukaa nao kwa wema bila ya kuwadhuru, na pia mnaweza kuwaacha watimize eda zao kwa kuzingatia muamala mwema ulio laiki wakati wa kufarikiana bila ya kuwatendea mabaya. Wala haijuzu katika kuwarejea ikawa makusudio yake ni madhara na kuirefusha eda. Mwenye kutenda hayo basi mwenyewe amejinyima starehe ya maisha ya mke na mume, na imani ya watu kwake, na anastahiki kukasirikiwa na Mwenyezi Mungu. Wala msizifanyie maskhara na mchezo na kuwa ni upuuzi hukumu za Mwenyezi Mungu zilizo kuja katika Aya hizi kwa ajili ya kutengeza maisha ya kinyumba, na zikaweka khatamu za ukoo katika mikono ya wakili, naye ni mume, mkawa mnatoa T'alaka bila ya sababu, na mkawapatisha wake zenu madhara na maudhi. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu kwa kukupangieni mpango bora kabisa katika maisha ya ndoa, na pia kwa aliyo kuteremshieni katika Kitabu kilicho bainisha wazi ujumbe wa Muhammad, na ilimu mbali mbali zenye manufaa, na mifano na hadithi za kukuwaidhini na kukuongoeni. Na jikingeni na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Jueni kuwa Mwenyezi Mungu anajua siri zenu na mnayo dhihirisha na niya zenu na vitendo vyenu. Naye ni Mwenye kukulipeni kwa myatendayo.
Mmnapo waacha wake na zikatimia eda na akitaka mwanamke kuanza maisha mapya kwa kuolewa tena ama na yule mku-mwenziwe au na mwanamume mwengine, basi si halali kwa wazee wala yule mku-mwenza kuwakataza, ikiwa pande mbili zimeridhiana kufanya ndoa mpya kwa kutaka maisha bora yatakayo pelekea masikilizano mema baina yao. Anawaidhiwa hayo anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Mwendo huo unapelekea kukuza mahusiano ya hishima na sharaf katika jamii zenu, na ni usafi zaidi katika nafsi zenu kut'ahirika na uchafu na mahusiano yaliyo maovu. Na Mwenyezi Mungu anajua maslaha ya binaadamu na siri za nafsi zao ambazo wao hawajui vipi kuzipata.
Ni juu ya kina mama kuwanyonyesha wana wao muda wa miaka miwili iliyo timia kwa maslaha ya mtoto mchanga, akitaka hayo mmojapo au wote kati ya wazazi. Itamlazimu baba, kwa kuwa mtoto ni wake, amkimu mama kwa chakula na nguo kwa uwezo wake bila ya israfu wala uchoyo. Kwani haimlazimu mtu kufanya ila kiasi ya uwezo wake, na wala haitakikani kumletea madhara mama kwa kumnyima haki yake ya kumkimu yeye na kumlea mwana. Kadhaalika haitakikani mtoto awe sababu ya kumletea madhara baba yake kwa kumkalifu zaidi kuliko uwezo wake, au kumharimisha haki yake kwa mwanawe. Na akifa baba au akawa fakiri hawezi kazi kiamu kitakuwa juu ya mrithi wa mtoto ikiwa mtoto ana mali yake. Wakitaka wazazi kumwachisha ziwa mtoto kabla ya kutimia miaka miwili wakakubaliana kwa hayo na huku wakiangalia maslaha ya mtoto basi hapana ubaya. Na nyinyi wazazi mkitaka kumpa mama mwingine kumnyonyesha mtoto pia hapana ubaya - na hapo mtamtolea ujira kwa ridhaa na ihsani. Katika myatendayo muangalieni Mwenyezi Mungu, na mjue kuwa Yeye anayajua myatendayo na atakulipeni kwayo. Qur'ani inawajibisha mama amnyonyeshe mwanawe na asinyonyeshwe na mwingine ila kwa dharura, kwani kunyonyesha yeye ni faida kwa mama na mtoto katika siha. Na kuachisha ziwa kuwe kwa taratibu, na yajuzu kabla ya kutimiza muda ikiwa siha ya mtoto inaruhusu hayo