Na wenye kumcha Mwenyezi Mungu hawana dhambi katika dhambi za hawa madhaalimu, ikiwa wataendelea na upotovu wao. Lakini yapasa kuwasemeza na kuwakumbusha, asaa huenda wakaiogopa adhabu ya Mwenyezi Mungu, na wakaacha upotovu.
Na ewe Nabii, waachilie mbali wale walio fanya sharia yao, mwendo wao, pumbao na mchezo, na wakakhadaika na maisha ya dunia wakaacha ya Akhera. Na daima kumbusha kwa Qur'ani, na wahadharishe vitisho vya Siku ambayo nafsi itafungika na a'mali yake, itapo kuwa hapana wa kunusuru wala wa kusaidia isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Na kila fidia ya kujiokoa haitokubaliwa. Hao makafiri watafungwa katika adhabu kwa sababu ya shari waliyo itenda. Katika Jahannamu watapewa kinywaji kimoto mwisho wa umoto, na adhabu chungu mno kwa sababu ya kufuru zao.
Waambie hawa makafiri kwa kuwasibabi: Je, inasihi kuwa tumuabudu asiye kuwa Mwenyezi Mungu, asiye weza kutuletea nafuu wala dhara? Na turejee kwenye shirki baada ya kuwa Mwenyezi Mungu kesha tupa tawfiqi ya kufikia Imani? Na tuwe kama aliye zugwa na mashetani na wakampoteza katika ardhi, akawa yuko katika pweleo lisilo weza kumwongoa kufuata Njia iliyo nyooka, na hali anao marafiki walio ongoka nao wanajaribu kumwokoa atoke kwenye upotofu, huku wakisema: Rejea kwenye njia yetu iliyo sawa; naye akawa hawaitikii!! Sema ewe Nabii: Hakika Uislamu ndio uwongofu na ndio uwongozi, na vyenginevyo ni upotofu tu. Na Mwenyezi Mungu ametuamrisha tuufuate Uislamu. Naye ndiye Muumba wa viumbe vyote, na ndiye Mwenye kuviruzuku, na Mwenye kupanga mambo yao.
Waachilieni mbali hao washirikina baada ya kuwa mmewaita kwenye uwongofu, na nendeni kwenye ibada ya Mola wenu Mlezi. Na timizeni SWala kwa njia ya unyenyekevu ulio kamilika kabisa. Na mkhofuni Mwenyezi Mungu, na timizeni amri zake. Kwani kwake Yeye ndio mtakusanywa nyote nyinyi.
Na ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi, na akasimamia uumbaji wake kwa Haki na hikima. Na wakati wowote Mwenyezi Mungu akitaka kiwe kitu kinakuwa papo hapo. Vitu huwa kwa neno: "Kuwa". Na kila neno lake ni la kweli na la haki. Na Yeye peke yake ndiye Mwenye uweza wa kutenda usio na ukomo Siku ya Kiyama, siku litapo pulizwa barugumu la kutangazwa ufufuo. Naye, Subhanahu, ndiye Mwenye kutulia juu ya ujuzi wake wa mambo yaliyo fichikana na yanayo onekana. Na ndiye anaye endesha mambo yake yote kwa hikima, na ndiye Mwenye kukusanya katika ujuzi wake mambo yaliyo fichikana na mambo yaliyo dhihiri.