Na Yeye ndiye anakulazeni usiku, na anakuamsheni mchana. Na anajua mnayo yachuma, mpaka utimie muda wa kumfikia kila mmoja wenu ajali yake duniani ya kufa. Kisha Siku ya Kiyama mtarejeshwa nyote nyinyi kwa Mwenyezi Mungu peke yake. Tena atakwambieni a'mali zenu mlizo tenda duniani, njema au mbaya, na akulipeni kwazo.
Naye ndiye Mwenye kushinda kwa uwezo wake, aliye tukuka kwa ufalme wake juu ya waja wake, na anaye kupelekeeni Malaika wa kudhibiti kila vitendo vyenu, mpaka ufike mwisho wa kila mmoja wenu, ishikwe roho yake na Malaika wetu tunao wapeleka kwa kazi hiyo. Na wao hao Malaika hawafanyi taksiri katika kazi walio wakilishwa kuitenda.
Tena hawa maiti watafufuliwa Siku ya Kiyama, na watasimamishwa mbele ya Mola Mlezi wao ambaye ndiye anayatawala mambo yao peke yake. Jueni kuwa Yeye tu ndiye wa kuamua baina ya viumbe na kuwahisabu katika Siku hiyo, naye ni Mwepesi wa kuhisabu na kulipa.
Ewe Nabii! Waambie washirikina: Nani anaye kuvueni na vitisho vya bara na baharini vinapo kutokeeni, mkamuaungukia na mkamwomba kwa unyenyekevu wa dhaahiri na wa ndani, mkisema: Tunaapa! Kama ukituvua na vitisho hivi tutakuwa katika wanao kiri fadhila yako, na wanao dumu kukushukuru?
Sema: Ni Allah, Mwenyezi Mungu wa pekee, ndiye aliye kuokoeni na vitisho hivi, na kila shida nyengineyo. Na kisha nyinyi pamoja na hayo mnamshirikisha na wengine katika ibada, ambao hawawezi kuondoa shari wala kuleta kheri!
Sema: Hakika ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye awezaye kukuleteeni adhabu kutoka juu yenu au chini yenu, au kukufanyeni nyinyi kwa nyinyi mkawa maadui, mkawa mataifa yenye kuwa mbali mbali matamanio yao, yenye kuchukiana, mkitesana nyinyi kwa nyinyi kwa mateso machungu na makali! Angalia vipi hoja zinavyo onyesha uwezo wetu na kustahiki kwetu peke yetu kuabudiwa, ili wapate kuzingatia na kuifahamu Haki.
Na kaumu yako wameikanusha Qur'ani, nayo ni Haki ambayo haina cha kukanushwa ndani yake. Ewe Nabii! Waambie: Mimi sikuwekwa kuwa ni muwakilishi wa kukulindeni, na kupima vitendo vyenu na kukulipeni kwavyo. Bali mambo yenu katika hayo yako kwa Mwenyezi Mungu.
Na ukihudhuria katika baraza za makafiri, ukawakuta wanazikosoa Aya za Qur'ani, au wanazifanyia maskhara, basi wewe waepuke mpaka watapo ingia katika mazungumzo mengine. Na ukisahau na ukakaa nao wakati wa mazungumzo yao hayo mapotovu, kisha ukaikumbuka amri ya Mwenyezi Mungu ya kujitenga nao, basi usikae tena na watu madhaalimu baada ya kukumbuka.