Na lau kuwa tunge jaalia huyo wa kumuunga mkono Mtume ni Malaika kama watakavyo hao, basi tungeli mfanya katika sura ya mwanaadamu, ili wapate kumwona na kufahamiana naye. Kwani wao hawawezi kumwona Malaika katika sura yake ya asili. Tena mambo yangeli watatiza na kuwadanganyikia kwa kupelekwa kwa sura ya mwanaadamu, na tungeli watia katika makosa yale yale yalio wazonga. Kauli hii inaashiria maana ambayo wenye ilimu za kisasa wanaitaja. Wenye ilimu za mambo ya kiroho wanasema kuwa roho zina mwili khafifu, mwembamba na mwepesi, mfano wa ng'amba. Nazo hazidhihiri wala hazionekani. Na hayumkiniki kuonekana roho ila zikivaa huo mwili. Na Malaika hawana kiwiliwili. Katika viumbe vyote vya kiroho Malaika ndio khafifu kabisa kushinda vyote. Na hayumkini kuonekana ila kwa sura ya mwili. Na huu mwili ndio unakuwa kama mwanaadamu.
Ewe Nabii! Makafiri waliwafanyia maskhara mengi Mitume wa kabla yako. Adhabu waliyo waonya nayo Mitume wao iliwazunguka hao wafanyao maskhara. Na kwanza hayo ndio waliyo kuwa wakiyakejeli.
Ewe Nabii! Waambie hawa makafiri: Nendeni pande zote duniani, mzingatie vipi maangamio yalivyo kuwa mwisho wa wanao wakanusha Mitume wao. Uzingatieni vyema mwisho huu na khatima hiyo.
Ewe Nabii! Waambie hawa wapinzani: Nani Mmiliki mbingu na ardhi, na viliomo ndani yao? Wakiemewa, wape jawabu ambayo hakuna nyengineyo, nayo ni: Hakika Mwenye kuvimiliki vyote hivyo ni Mwenyezi Mungu peke yake, wala hana mshirika. Na Yeye amejiwajibishia Mwenyewe rehema kuwarehemu waja wake. Kwa hivyo hawafanyii haraka kuwaadhibu, na anakubali toba yao. Hakika, atakukusanyeni Siku ya Kiyama ambayo haina shaka. Walio zipoteza nafsi zao, na wakazipelekea kwenye adhabu katika Siku hii, ni wale ambao hawamsadiki Mwenyezi Mungu, wala Siku ya Hisabu.
Ni vya Mwenyezi Mungu vya kila zama, kama ilivyo kuwa vyake vya kila pahala. Naye ndiye Mwenye kusikia kila la kusikiwa, na Mwenye kujua kila la kujuulikana.
Sema ewe Nabii! Mimi simfanyi yeyote kuwa ni mungu na msaidizi isipo kuwa Mwenyezi Mungu, Allah, tu. Yeye peke yake ndiye aliye ziumba tangu mwanzo mbingu na ardhi kwa nidhamu isiyo kuwa na kiigizo kilicho tangulia. Naye ndiye Mwenye kuwaruzuku chakula waja wake, wala Yeye hahitaji kwao chakula. Sema: Hakika Mwenyezi Mungu ameniamrisha niwe wa mwanzo wa kusilimu, na amenikataza kumshirikisha Yeye na yeyote mwenginewe katika kumuabudu.
Mwenye kuepushwa adhabu hii Siku ya Kiyama, basi Mwenyezi Mungu amemrehemu. Na huko ndiko kufuzu kulio thibiti, kulio wazi.
Mwenyezi Mungu akikupatiliza kwa ovu, basi hapana wa kuliondoa hilo ila Yeye Mwenyewe. Na akikupa kheri basi hapana awezae kuirudisha fadhila yake, kwani Yeye ni Muweza wa kila kitu.
Yeye ndiye Mwenye kushinda kwa uwezo wake, Aliye juu, juu ya waja wake, Aliye sifika kwa hikima katika kila alifanyalo, Mwenye kuvizunguka kwa ujuzi wake vinavyo onekana na vinavyo fichikana.