Ikiwa hawa watapata adhabu hii, Waumini watapata Pepo na neema zake. Na hayo wamekwisha ahidiwa. Na hali ya Bustani walio ahidiwa wanao simama juu ya Haki na wakaweka kinga baina ya upotovu na Imani, ni kuwa itapitiwa chini ya miti yake maji matamu, na matunda yake ni ya daima hayasiti, na kivuli chake vilevile ni cha daima. Na haya ndiyo malipo ya wale wanao jikinga na shari. Ama makafiri wanao kanya, malipo yao ni kuingia Motoni.
Na wale ambao walio pewa ujuzi wa Vitabu vilivyo teremshwa ni waajibu wao wakifurahie Kitabu hichi ulicho teremshiwa wewe. Kwani hichi ni maendeleo ya ule ule ujumbe wa Mwenyezi Mungu. Na wanayo ifanya dini kuwa ni sababu ya kufanya makundi mbali mbali wanayakataa baadhi ya uliyo teremshiwa kwa uadui na chuki tu. Basi ewe Nabii! Waambie: Hakika mimi sikuamrishwa ila nimuabudu Mwenyezi Mungu, na nisimshirikishe katika ibada yake na kitu chochote. Na kwendea kumuabudu Yeye peke yake ndio ninalingania, ninaita, na kwake Yeye peke yake ndio marejeo yangu.
Na kama vilivyo teremka Vitabu vya mbinguni, tumekuteremshia wewe hii Qur'ani ili iwe ni hakimu baina ya watu kwa yaliyo baina yao, na iwe ni hakimu wa Vitabu vilivyo tangulia kuwa ni vya kweli. Na hii Qur'ani tumeiteremsha kwa lugha ya Kiarabu. Wala usitake kuwafurahisha washirikina au Ahli Lkitab (watu wa Biblia), baada ya ufunuo na ilimu iliyo kufikia. Na ukitaka kuwaridhi basi hutakuwa na wa kukusaidia au kukulinda mbele ya Mwenyezi Mungu. Hapa anaambiwa Nabii, khasa wanasemezwa Waumini wote. Na mahadharisho ya Waumini ni kweli kweli hivyo; na kwa Nabii ni kwa ajili ya kubainisha kuwa juu ya kuwa yeye ni mteuliwa, na mtukufu wa daraja, bado anafaa kuhadharishwa.
Na ikiwa washirikina wanachochea watu wastaajabu kuwa wewe una wake na dhuriya, yaani wazao, na wanataka ulete muujiza mwengine usio kuwa Qur'ani, basi tulileta kabla yako Mitume wenye wake na wana vile vile. Kwani Mtume ni mwanaadamu, na ana sifa za kibinaadamu. Lakini yeye ni mbora kuliko wote. Wala Nabii hawezi kuleta muujiza kama apendavyo yeye au wapendavyo watu wake! Bali aletaye muujiza ni Mwenyezi Mungu, na Yeye ndiye anaye toa idhini. Kila kizazi katika vizazi kina amri yao aliyo waandikia Mwenyezi Mungu ya kuwasilihi. Na kila kizazi kina muujiza wake unao wanasibu. (Nabii Isa a.s. anasimuliwa katika Injili ya Yohana 5.30 kuwa alisema: Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe.)
Mwenyezi Mungu hufuta sharia na miujiza, na akaleta badala yake atakayo na akaithibitisha. Na kwake Yeye ipo asili ya Sharia zilizo thibiti zisio geuka, na ndio kwenye Umoja na asili ya fadhila zote, na mengineyo.
Na tukikuonyesha baadhi ya malipo au adhabu tulizo waahidi, au tukakujaalia ufe kabla ya hayo, ungeli ona kitisho kitacho washukia washirikina, na ungeli ona neema za Waumini! Lakini haya hayakukhusu wewe, juu yako wewe ni kufikisha Ujumbe tu, na kwetu Sisi peke yetu ndio hisabu.
Na hakika dalili za adhabu na kushindwa zipo! Hawaangalii kwamba Sisi tunazifikia nchi walizo kuwa wakizitawala zinachukuliwa na Waumini kidogo kidogo? Na kwa hivyo tunawapunguzia wao ardhi zilio wazunguka. Na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye wa kuhukumu kushinda na kushindwa, na thawabu na adhabu. Na wala hapana wa kuipinga hukumu yake. Na hisabu yake ni ya mbio mbio, haihitajii kupitiwa na wakati mrefu, kwani Yeye ni Mjuzi wa kila kitu. Basi ishara zipo! Aya hii ina ukweli ulio fikiliwa na uchunguzi wa kisayansi za hivi sasa, ya kwamba imethibiti kuwa dunia inazunguka, na kuwa inayo mvuto kama simaku. Hayo yamepelekea kubabataa katika ncha mbili za kaskazini na kusini, North Pole na South Pole. Na hivyo ni kupunguka katika ncha mbili za ardhi. Na kadhaalika imejuulikana kuchopoka mbio za sehemu za gasi zilizo funika huu mpira wa dunia kukipindukia nguvu za mvuto wa ardhi, basi hutoka nje ya dunia. Na haya yanatokea mfululizo, na kwa hivyo ardhi, yaani dunia, inakuwa katika hali ya kupunguka moja kwa moja katika ncha zake. Haya yanakuwa kwa kuifasiri ardhi kuwa ni dunia, si nchi ya maadui wa Waumini. Yaelekea taf siri hii kwa Aya hii tukufu, ijapo kuwa wafasiri wengi wamefasiri kuwa muradi wa "ardhi" ni nchi za maadui.
Na walio kuwa kabla yao waliwapangia Mitume wao mipango ya uwovu. Lakini Mwenyezi Mungu Subhanahu ndiye Mwenye mipango yote kwa makafiri walioko sasa na walio watangulia. Na watapata malipo kwa wanayo yatenda, na Yeye anayajua ayatendayo kila kiumbe. Na ikiwa wao hawajui kuwa mwisho mwema ni wa Waumini, basi Siku ya Kiyama watajua kwa kuona nani atapata mwisho mwema kwa kukaa katika Nyumba ya neema.