Na huko kupita mpaka upotovu kunawapelekea kutaka wateremshiwa adhabu haraka haraka badala ya kuomba hidaya itayo waokoa. Na wanadhani kwamba Mwenyezi Mungu hawateremshii adhabu duniani akitaka. Na zimekwisha wapitia adhabu watu mfano wao kwa hayo, katika alio wateketeza Mwenyezi Mungu kabla yao. Lakini ni shani ya Mwenyezi Mungu kusamehe dhulma ya mwenye kutubia akarejea kwenye Haki, na kumteremshia adhabu kali anaye endelea na upotovu.
Na husema hao makafiri wasio amini muujiza mkubwa, yaani Qur'ani: Hebu na amteremshie Mola wake Mlezi alama ya unabii wake wa kuonekana kama kuiendesha milima akawa Mwenyezi Mungu anaonyesha wazi uhakika wa Nabii wake katika jambo hili! Na Yeye Subhanahu anamwambia: Hakika wewe ni Nabii wa kuwaonya kwamba kuna adhabu mbaya wakiendelea na upotovu wao. Na kila kaumu wanaye Mtume wa kuwaongoza kwenye Haki, na muujiza wa kubainisha ujumbe wake. Si wao wa kuchagua. Lao ni kujibu upinzani na kuleta mfano wake!
Aliye mpa Mtume huo muujiza mkubwa kabisa ni Yeye anaye jua kila kitu, na anazijua nafsi za binaadamu tangu kuumbwa kwao kutokana na mbegu za uzazi katika tumbo la mama mpaka wakati wa kufa kwao. Basi Yeye anaijua mimba anayo ichukua kila mwanamke kama ni mume au mke, kinacho punguka tumboni na kilicho zidi wakati, mpaka utimie muda wa mimba, na mtoto akamilike kukua, azaliwe. Kila kitu kwake Yeye Subhanahu kina kipimo maalumu, na muda maalumu.
Yeye anayajua ya ghaibu tusiyo yahisi, na tunayo yashuhudia kwa ujuzi zaidi kuliko tunavyo shuhudia sisi na kuona. Na Yeye Subhanahu ni Mwenye shani kubwa iliyo tukuka juu ya kila kiumbe.
Anazijua hali zenu zote katika maisha yenu, na maneno yenu na vitendo vyenu vyote. Basi anayajua mnayo yaficha na mnayo yatangaza, vitendo na maneno. Na anajua vile mnavyo jificha usiku na kujitokeza mchana. Na yote ni sawa katika ujuzi wake.
Na Mwenyezi Mungu Aliye takasika ndiye anaye kuhifadhini. Kila mtu anao Malaika wanao mlinda kwa amri ya Mwenyezi Mungu, na wanapeana zamu kumlinda mbele na nyuma yake. Na hakika Mwenyezi Mungu Subhanahu habadilishi hali ya watu kutoka shida kwendea neema, na kutoka nguvu wakawa dhaifu, mpaka wao wenyewe wageuze waliyo nayo kufuatana na hali wanayo iendea. Na Mwenyezi Mungu akitaka kuwateremshia watu maovu basi hawana wa kuwanusuru ataye walinda na amri yake, wala wa kuwatazamia mambo yao kuwakinga na yatayo wateremkia.
Na uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika ulimwengu unaonekana wazi, na athari zake zipo dhaahiri. Ni Yeye anaye kuonesheni umeme, ukakutisheni kuuona au mkakhofu isikujieni mvua wakati msio ihitaji ikakuharibieni mazao, au mkatumai kwa umeme itakuja mvua kubwa mnayo ihitajia kwa maslaha ya ukulima. Ni Yeye anaye yafanya mawingu yaliyo jaa mvua.
Na hakika radi zinamnyenyekea Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la kwa unyenyekevu ulio timia, mpaka ikawa sauti yake mnayo isikia ni kama kwamba inamtakasa na kumsabihi kwa kumhimidi, kumsifu na kumshukuru, kwa kuumba kwake kama ni ishara ya unyenyekevu wake. Na vile vile Roho safi msizo ziona, yaani Malaika, pia zinamtakasa Yeye. Na Yeye ndiye anaye peleka moto wa radi unao unguza ukampata amtakaye. Na juu ya kuwepo ishara hizi zinazo onekana zenye dalili ya uwezo wake Subhanahu wao bado wanabisha shani ya Mwenyezi Mungu Aliye takasika. Na Yeye ni Mwenye nguvu kubwa za kuvipinga vitimbi vya maadui.