Ewe Nabii! Yakikusibu madhara kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hapana wa kuyaondoa ila Yeye. Na akikujaalia kheri hapana anaye weza kukunyima yeyote. Kwani yeye anagawa kheri kuwapa waja wake kwa fadhila yake. Na Yeye Subhanahu ni Mkunjufu wa maghfira, Mkuu wa rehema.
Ewe Mtume! Fikisha wito wa Mwenyezi Mungu kwa watu wote! Na waambie: Enyi watu! Hakika Mwenyezi Mungu amekuteremshieni Sharia ya Haki kutokana naye. Anaye taka kuongoka basi afanye haraka. Kwani faida ya uwongofu wake utamrejea mwenyewe. Na mwenye kushikilia upotovu utamuangukia mwenyewe. Na mimi sikuwakilishwa nikulazimisheni muamini, wala kukutawalini.
Ewe Mtume! Thibiti juu ya Dini ya Haki. Na fuata wahyi ulio teremshiwa, nawe uwe na subira kwa maudhi yanayo kufika kwa ajili ya Njia ya Da'wa (Wito), mpaka Mwenyezi Mungu ahukumu baina yako na wao, kwa vile alivyo kuahidi kuwa atawapa ushindi Waumini, na watahizika makafiri. Na Yeye ndiye mbora wa mahakimu.