Harufi hizi - Alif Lam Raa - ni sawa na A.L.R. Mwenyezi Mungu Mtukufu ameanzia Sura hii. Na Yeye ndiye anajua muradi wake. Na juu ya hivyo zinaashiria kuwa Qur'ani imeundwa kwa harufi hizi hizi za Alifbete, na nyinyi mmeshindwa kuleta mfano wake! Na kwa harufi hizi za kutamkwa zinawazindua washirikina, wakawa wanasikiliza, ijapo kuwa wanawafikiana kuwa wasizisikilize Aya Tukufu hizi na mfano wake ambazo ni Aya za Qur'ani yenye hikima katika mpango wake na maana zake, na ambayo imekusanya hikima na kila linalo wanafuisha watu katika Dini yao na dunia yao.
Haiwafalii watu kustaajabu wakakanusha wahyi wetu tunao mfunulia mtu mmoja wao, naye ni Nabii Muhammad s.a.w., ili awahadharishe watu na adhabu ya Mwenyezi Mungu, na awape bishara njema wale miongoni mwao walio amini, ya kwamba hapana shaka yoyote wana cheo kitukufu cha juu kwa Mola wao Mlezi. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu haigeuki. Wala haiwafalii hao watu wakanushi kumsema Muhammad, Mtume wetu, kuwa yeye ni mchawi maarufu.
Enyi watu! Hakika Mola wenu Mlezi ni Mwenyezi Mungu aliye umba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake katika siku sita ambazo kipimo chake hakijui ila Mwenyezi Mungu. Akatandaza utukufu wa utawala wake, peke yake, na akayapanga mambo yote ya viumbe vyake. Basi hapana yeyote mwenye chochote pamoja na utawala wa Mwenyezi Mungu. Wala hawezi yeyote katika viumbe vyake hata kumwombea mtu isipo kuwa kwa ruhusa yake. Huyo, basi, ndiye Mwenyezi Mungu Muumba, huyo ndiye Mola wenu Mlezi, na ndiye Mlinzi wa neema zenu. Basi muabuduni Yeye peke yake, na msadikini Mtume wake, na kiaminini Kitabu chake. Juu yenu kukumbuka neema za Mwenyezi Mungu, na zingatieni Ishara zake zinazo thibitisha Upweke wake. Mwenyezi Mungu ameumba viumbe vyote kwa vipindi sita, na vipindi hivi ni viwango vya mamilioni ya makarne na makarne. Na hivyo ndivyo vinavyo itwa Siku Sita. Na katika kila nguzo za ulimwengu zipo Ishara wazi zilizo zagaa za kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Miongoni mwa hizi, ni hivi kufanywa jua na mwezi na nyota kunyenyekea kwa faida ya binaadamu. Na kadhaalika kupishana zamu usiku na mchana, na kuwa mchana unaingilia kiza cha mbingu. Na umetajwa usiku mbele kwa kuwa kiza ndio asli. Ama mchana umezuka kwa kuathirika kwa mwangaza wa jua katika anga la ardhi, ambayo hiyo ardhi inazunguka wenyewe kwa wenyewe kama pia ili ipate mwangaza wa jua, mara upande huu na mara upande huu
Kama Mwenyezi Mungu alivyo anzisha uumbaji wa viumbe peke yake, basi marejeo yenu, na marejeo ya viumbe vyote ni kwake Yeye. Na Mwenyezi Mungu ameahidi hivyo kwa ahadi ya kweli isiyo na khitilafu. Na hakika Yeye Subhanahu ameanzisha kuumba viumbe kwa kudra yake, na vitapo teketea atavirejesha kwa kudra yake, ili awalipe Waumini wenye kumt'ii thawabu kwa uadilifu ulio timia. Ama makafiri, wao huko katika Jahannamu watapewa vinywaji vinavyo tokota kweli kweli, na watapata adhabu yenye kutia machungu kuwa ni malipo ya ukafiri wao.
Na Mola wenu Mlezi ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi, na akalifanya jua litoe mwanga, na mwezi utoe nuru. Na akajaalia mwezi uwe na vituo ili vikusaidieni kuweza kupima nyakati zenu, na mjue idadi ya miaka na hisabu. Na wala Mwenyezi Mungu hakuumba hayo ila kwa hikima. Na Yeye Subhanahu katika Kitabu chake anazikunjua Ishara zenye kuonyesha Ungu wake na ukamilifu wa uwezo wake, ili mpate kuzingatia kwa akili zenu, na mkubali kwa yanayo hitajia ujuzi. Aya hii ya 5 inahakikisha ukweli wa kisayansi ambao haukujuulikana na hiyo sayansi ila hivi mwishoni. Hapo kwanza haukujuulikana, nao ni kuwa jua ni umbo lenye kuwaka moto, na ndio chanzo cha nguvu za kufanyia kazi zote, kwa Kiarabu huitwa T'aaqa, na kwa Kiingereza Energy, na kwa Kiswahili cha sasa Nishati. Katika nguvu hizo ni huo Mwangaza na Joto. Ama mwezi hauwaki moto, bali unarudisha mwangaza wa jua, kama kioo, kwa hivyo huonekana una nuru. Kwa hivyo Subhanahu ameeleza kuwa jua lina mwangaza wa asli, na mwezi unatoa nuru tu. Na Aya hii imeashiria hakika ya nyendo za falaki, nayo ni kuwa mwezi unaizunguka ardhi, na kila siku unakuwa katika mahala fulani kwa mintarafu ya dunia. Ukimaliza mzunguko wake ndio unatimia mwezi, huu wa siku 30 au 29. Kwa hivyo tunaweza kujua kiasi cha mwaka, na kwa hivyo twaweza kujua hisabu za miaka, miezi na siku.
Hakika katika kufuatana usiku na mchana na kukhitalifiana kwao, kwa kuzidi na kupungua, na katika uumbaji wa mbingu na ardhi na vitu vyote viliomo humo, zipo dalili zilizo wazi na hoja zilizo dhaahiri zenye kuhakikisha Ungu wa Mwenye kuumba, na uwezo wake. Hayo ni kwa wenye kutaka kuiepuka ghadhabu yake na wakaiogopa adhabu yake. Aya hii ya 6 inaashiria hakika inayo onekana, nayo kukhitalifiana urefu wa usiku na mchana kwa mwaka mzima katika pahala popote duniani. Na kadhaalika kufuatana mchana na usiku, na kuwa mchana ni wa kuangaza na kuonana, na usiku ni giza. Na maana ya hayo ni kuwa msingi wake ni kuwa dunia inazunguka wenyewe kwa wenyewe kama pia juu ya msumari wake, na vile vile inalizunguka jua. Na yote hayo ni dalili ya uwezo wa Mwenye kuumba katika kuanzisha uumbaji. Ujuzi wa mambo hayo wakati wa Mtume s.a.w. haukuwepo. Na hii ni dalili nyengine ya kwamba haya hayakuwa ila ni wahyi, ufunuo, ulio toka kwa Mwenyezi Mungu kumpa Mtume s.a.w.