Na Mwenyezi Mungu hawapendi wanao toa mali kwa ajili ya kuonekana na watu, wapate kuwasifu na kuwatukuza, na ilhali wao si wenye kumuamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Malipo. Kwani hao wamemfuata Shetani naye amewapoteza. Na mwenye kuwa rafiki yake ni Shetani basi ana rafiki mbaya kweli.
Ama wamelaanika watu hawa! Kingewadhuru nini wao lau kuwa wamemuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Akhera, na wakatoa katika alicho wapa Mwenyezi Mungu kwa kufuatana na Imani hii, na usafi wa niya, na kutaraji thawabu kama ilivyo wajibikia? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kwa ujuzi kaamili mambo yote yaliyo wazi na yaliyo fichikana ndani.
Hakika Mwenyezi Mungu hamdhulumu mtu hata kidogo. Basi hampunguzii ujira wake mtu, wala adhabu yake hamzidishii kabisa. Bali humzidishia mtenda mema thawabu zake mardufu hata zikiwa kidogo vipi. Na humpa kwa fadhila yake malipo makubwa yasiyo lingana na hayo mema yake ambayo yamekwisha zidishwa mardufu.
Vipi basi itakuwa hali ya hao mabakhili wanao pingana na aliyo yaamrisha Mwenyezi Mungu, tutapo mleta Siku ya Kiyama kila Nabii awe ni shahidi juu ya kaumu yake, na tukakuleta wewe, ewe Nabii Muhammad, kuwa ni shahidi juu ya kaumu yako, na hali miongoni mwao wapo hao wanao zuia mali yao na wanao pinga?
Yatapo tokea haya watatamani hao wapinzani wanao pinga lau kuwa wangeli potea chini ya Ardhi kama wanavyo potea maiti makaburini! Na wao hawawezi kumficha Mwenyezi Mungu kitu chochote katika mambo yao, na hali zao na vitendo vyao vitadhihiri.
Enyi mlioamini! Msende kusali misikitini nanyi mmo katika hali ya ulevi mpaka muwe mnafahamu myasemayo. Wala msiingie misikitini nanyi mna janaba, ila ikiwa ni kupita njia tu bila ya kusita, mpaka mtahirike kwa kukoga. Na mkiwa ni wagonjwa hamuwezi kutumia maji kwa kuogopa maradhi yasikuzidini au kuchelewa kupona, au mkiwa mmo safarini na ipo shida ya kupata maji, basi tumieni mchanga ulio safi. Kadhaalika mmoja wenu akitoka chooni, au mkawaingilia wanawake na mkawa hamkupata maji ya kujitahirishia kwa kukosekana kwake, basi vile vile chukueni mchanga safi upigeni kwa mikono yenu, na mpangusie nyuso zenu na mikono yenu. Hakika ni shani ya Mwenyezi Mungu kuwa ni Mwenye kusamehe sana na Mwenye kufuta dhambi.
Hebu huyastaajabii mambo ya hawa walio pewa sehemu ya Vitabu vilivyo tangulia wanavyo acha uwongofu na wakatafuta upotovu katika mambo yaliyo wakhusu nafsi zao! Na wao tena wanakutakeni nyinyi mjitenge na Haki ambayo ndiyo Njia ya Mwenyezi Mungu Iliyo Nyooka!