Ili uwaonye watu ambao baba zao wa karibu hawakupata kuonywa, na kwa hivyo wamesahau yanayo wajibikia kwa Mwenyezi Mungu, na kwa nafsi zao, na kwa watu.
Sisi tulikwisha jua kuwa wengi wao hawatakhiari Imani. Basi yale tuliyo kuwa tunayajua yamewafikiana na yaliyo kwao. Basi haitakuwapo Imani kutoka kwao.
Sisi tumewafanya hao wanao kakamia juu ya ukafiri ni kama walio tiwa minyororo shingoni mwao, ikawafika videvuni mwao. Na mikono yao ikawa imefungwa kwenye vichwa vyao, vikawa vimenyanyuka juu na macho yao yameinama. Basi hawawezi kuvizungusha vichwa vyao wapate kuona.
Na tumewafanya wale walio zuwiwa wasione Ishara na dalili ni kama walio fungwa baina ya kuta mbili, na macho yao yakagubikwa, wasione yaliyo mbele yao wala yaliyo nyuma yao.
Hakika wanao nafiika kwa kuhadharisha kwako ni wale wanao ifuata Qur'ani na wakamkhofu Arrahman, ijapo kuwa hawamwoni. Basi watu hawa wape bishara njema kuwa Mwenyezi Mungu atawasamehe madhambi yao, na atawalipa malipo mema kwa vitendo vyao.
Hakika Sisi tunawahuisha maiti, na tunayaandika yote waliyo yatenda na wakayakadimisha duniani, na walio yabakisha humo kuwa ni athari, mabaki, yao baada ya kufa kwao. Na kila kitu kimo katika Kitabu kilicho wazi.