Mimi nimeacha mila ya hawa makafiri, na nikafuata Dini ya baba zangu Ibrahim, na Is-haaq, na Yaa'qub. Nikamuabudu Mwenyezi Mungu pekee. Haitufalii sisi kumfanyia Mwenyezi Mungu mshirika yeyote yule, akiwa Malaika, au jini, au mwanaadamu, licha ya masanamu ambayo hayaleti manufaa wala madhara, wala hayasikii, wala hayaoni! Hiyo ndiyo Tawhidi aliyo tutunukia Mwenyezi Mungu sisi na watu wote, kwa vile alivyo tuamrisha tuwafikilishie ujumbe. Lakini wengi wa watu hawaipokei fadhila hii kwa shukrani, bali wanaikataa!
Enyi wenzangu wawili wa gerezani! Je mabwana wengi mbali mbali ni bora mtu kuwanyenyekea kuliko Mwenyezi Mungu Mmoja asiye shindika?
Hamuabudu badala ya Mwenyezi Mungu ila majina tu mliyo yazua nyinyi na baba zenu kwa mawazo bila ya kuwepo kweli. Mwenyezi Mungu hakuwateremshia hao hoja wala ushahidi wowote! Hapana wa kuhukumu nini kinacho faa kuabudiwa na kipi hakifai ila Mwenyezi Mungu tu. Yeye ameamrisha msimnyenyekee yeyote mwenginewe, na mumuabudu Yeye peke yake. Hiyo ndiyo Dini iliyo nzima iliyo nyooka, ambayo dalili zote na ushahidi unaelekea kwake. Lakini aghlabu ya watu hawataki uwongozi wa dalili hizi, wala hawajijui kuwa wamo katika ujinga na upotovu.
Enyi wenzangu wawili wa gerezani! Hii basi ndiyo tafsiri ya ndoto zenu: Ama mmoja wenu aliye kamua zabibu katika ndoto yake, atatoka jela, na atakuwa akimnywesha mvinyo Mfalme. Na ama huyu wa pili atatundikwa msalabani, na ataachwa msalabani ndege wakimla kichwa chake. Yamekwisha timia hayo mambo kama nilivyo eleza kwa mujibu mlivyo nitaka nieleze tafsiri ya hizo ndoto!
Akamwambia yule aliye kuwa atavuka: Nitaje kwa Mfalme kwa sifa zangu, na kisa changu. Asaa huenda akanifanyia insafu akanivua na haya mateso! Shetani alimshughulisha akamsahaulisha kutaja kisa cha Yusuf kwa Mfalme. Basi Yusuf akabaki gerezani kwa miaka isiyo pungua mitatu.
Mfalme akasema: Nimeota usingizini kuna ng'ombe saba wanene wanaliwa na wengine saba walio konda madhaifu. Na nimeota mashuke saba mabichi, na mengine saba makavu. Enyi wakuu wanazuoni na wenye maarifa! Nitoleeni fatwa ya hizi ndoto zangu, ikiwa ni kweli nyinyi mnajua tafsiri za ndoto na mnaweza kuzitolea fatwa.