Hakika msaidizi wangu wa kuninusuru nanyi ni Yeye Mwenyezi Mungu. Ulinzi wangu uko kwake. Naye ndiye aliye niteremshia Qur'ani. Na Yeye peke yake ndiye anaye wanusuru waja wake walio wema.
Na hayo masanamu mnayo taka kwao msaada, badala ya Mwenyezi Mungu, hayawezi kukusaidieni nyinyi, wala kujisaidia wenyewe.
Na ukiwataka uwongofu katika yaliyo na kheri nanyi hawalisikii ombi lenu, licha ya kukuongozeni! Unawaona wanavyo kukabili kama kwamba wanakutazama, na kumbe wao kwa hakika hawaoni kitu!
Ewe Nabii! Waachilie mbali hao majaahili, na endelea katika njia ya Da'wa (Wito). Na wachukulie watu kwa lilio wepesi kwao. Na waamrishe kila jambo linalo pendeza na kuingia akilini.
Na Shetani akikuchochea kwa wasiwasi ili apate kukuachisha ulio amrishwa, kama vile kukasirika kwa kukushikilia kwao mambo ya shari, basi omba ulinzi wa Mwenyezi Mungu akuepushe naye huyo Shetani. Kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na kujua kila linalo tokea.
Hakika wale wamchao Mola wao Mlezi, na wakaweka baina yao na maasi kinga cha kuzuia uchochezi wa Shetani unao wapitia kuwaachisha yaliyo waajibu wao, hukumbuka uadui wa Shetani na vitimbi vyake. Kwa hivyo hao wanaiona Haki, basi ndio wanarejea.
Na usipo waletea makafiri Ishara wanayo itaka kwa inadi na ukafiri, husema: Kwa nini hukuitaka? (au hukuizua? Makusudio yao ni kuwa Mtume s.a.w. akizibuni Aya zote.) Waambie: Mimi sifuati ila Qur'ani ninayo funuliwa kwa wahyi kutoka kwa Mola wangu Mlezi. Na waambie: Hii Qur'ani ni hoja zinazo toka kwa Mola Mlezi wenu kukuonyesheni njia za Haki. Nayo ina uwongofu, na rehema, kwa Waumini, kwa sababu wao wanaifuata kwa vitendo.
Enyi Waumini! Mkisomewa Qur'ani isikilizeni kwa masikio yenu, mpate kuzingatia mawaidha yake, na msikilize vizuri mpate kuipata rehema.
Na mtaje Mola wako Mlezi ndani ya nafsi yako, upate kuhisi kuwa upo karibu na Mwenyezi Mungu, kwa kumnyenyekea na kumkhofu, bila ya kupiga makelele, bali juu kidogo kuliko kwa siri, na chini ya kudhihirisha kwa maneno. Na umtaje na umkumbuke asubuhi na jioni, ili uanzie mchana wako kwa kumkumbuka Mola wako Mlezi, na ukhitimishie kwayo vile vile. Na wakati wako wote usighafilike na kumtaja na kumkumbuka Mwenyezi Mungu.
Hao walio karibu na Mola wako Mlezi kwa utukufu na takrimu hawatakabari wakaacha kumuabudu. Na wanamtakasa Mwenyezi Mungu na kila lisio faa kwake. Na wanamnyenyekea Yeye.