Na tukadirie hapa duniani maisha mema, na tupate tawfiqi tuweze kut'ii, na Akhera tupate malipo mazuri, na maghfira, na rehema, kwa kuwa sisi hakika tumekwisha rejea kwako na tunatubu kwako. Mola Mlezi wao akawaambia: Adhabu yangu namfikishia nimtakaye katika wasio tubu, na rehema yangu imeenea juu ya kila kitu, na nitawaandikia khasa wale wanao jikinga na ukafiri na maasi katika kaumu yako, na wanao toa Zaka zilio lazimishwa, na wanao sadiki Vitabu vyote vilivyo teremka.
Na nawakusudia khasa wanao mfuata Mtume Muhammad, ambaye haandiki wala hasomi, na ambaye wanakuta sifa zake zimeandikwa katika vitabu vyao vya Taurati na Injili. Yeye anawaamrisha kila kheri na anawakataza kila shari. Na anawahalalishia vitu ambavyo tabia inaviona ni vizuri, na anawaharimishia vitu ambavyo tabia inavichukia kwa kuwa vina madhara, kama damu na mzoga. Na anawaondolea mizigo mizito na mikazo iliyo kuwa ikiwabana. Basi wanao usadiki Utume wake, na wakamsaidia, na wakamuunga mkono, na wakamnusuru na maadui zake, na wakaifuata Qur'ani aliyo teremshiwa pamoja naye kama nuru ya uwongofu, hao basi ndio wenye kufuzu, sio wenginewe ambao hawakumuamini.
Ewe Nabii! Waambie watu: Hakika mimi nimetumwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwenu nyinyi nyote, bila ya farka baina ya Mwaarabu na asiye kuwa Mwaarabu, baina ya mweusi na mweupe. Na Mwenyezi Mungu aliye nituma ni Yeye peke yake ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Huipitisha amri yake kwa mujibu wa hikima yake. Na hufanya mbinguni na duniani kama anavyo penda. Wala hapana wa kuabudiwa kwa haki ila Yeye. Na Yeye ndiye Mwenye uwezo wa kuhuisha na kufisha, wala hapana mwenginewe. Basi muaminini Yeye na Mtume wake, huyu Nabii asiye soma wala kuandika. Naye huyu anamuamini Mwenyezi Mungu ambaye anaye kuiteni mumuamini. Na anaamini Vitabu vyake vilivyo teremshwa. Basi mfuateni katika kila afanyalo na asemalo mpate kuongoka na kuongozeka.
Na katika kaumu ya Musa wako jamaa walio bakia na Dini iliyo sawa. Wakiwahidi watu kwa Haki aliyo kuja nayo Musa kutoka kwa Mola wake Mlezi, na wakifanya uadilifu pale wanapo pitisha hukumu.