Mwenyezi Mungu alipo mzuilia Musa asimwone, akaingia kumhisabia neema zake ili amliwaze kwa vile kumkatalia, akamwambia: Ewe Musa! Mimi nimekufadhilisha, na nimekuteua kuliko watu wote wa zama zako, ili ufikishe vitabu vya Taurati, na kwa kusema nawe bila ya kuwapo mtu kati. Basi yashike hayo niliyo kukufadhili, na unishukuru kama wafanyavyo wenye kushukuru, wanao kadiri neema.
Na tulimbainishia Musa katika zile mbao za Taurati kila kitu kilicho khusu mawaidha na hukumu zilizo elezwa mbali mbali, wanazo hitajia watu duniani na Akhera. Na tukamwambia: Zishike hizi mbao baraabara na kwa kuazimia. Na waamrishe watu wako washike yaliyo bora humo, kama kusamehe badala ya kulipiza kisasi, na kuachilia badala ya kungojea, na kulegeza badala ya kukaza. Enyi kaumu ya Musa! Nitakuonyesheni katika vitabu vyenu makaazi ya wale wanao asi amri za Mwenyezi Mungu, na watavyo angamia, ili mpate kuzingatia. Basi msende kinyume yakakusibuni yalio wasibu hao waasi.
Hao walio majeuri na wakapanda kiburi katika ardhi wakakataa kukubali yaliyo sawa bila ya haki, nitawazuia wasiweze kuzizingatia dalili za uwezo wangu ziliomo katika nafsi za watu na jiha zote. Watu hawa hata wakiona kila Ishara inayo thibitisha ukweli wa Mitume wetu hawaisadiki. Na wakiiona njia ya uwongofu hawaipiti, na wakiiona njia ya upotofu ndio wanaipita! Hayo yanatokea kwao kwa sababu wamezikanusha Ishara zetu zilio teremshwa, na wameghafilika na kuongoka kwazo.
Na walio zikanusha Ishara zetu zilio teremshwa juu ya Mitume wetu kwa ajili ya uwongofu, na wakakanusha kukutana nasi Siku ya Kiyama, wakakataa kufufuliwa na kulipwa, vitendo vyao walivyo kuwa wakitarajia viwafae vitapotelea mbali. Hawatokuta ila malipo ya kufru na maasi waliyo endelea nayo kuyatenda.
Na baada ya Musa kwenda kwenye mlima kusema na Mola Mlezi wake, kaumu yake walichukua vyombo vyao vya kujipamba wakatengeneza sura ya ndama, asiye na akili wala hatambui kitu. Lakini akitoa sauti mfano wa sauti ya ng'ombe, kwa namna walivyo muunda na ukipita upepo ndani yake. Na aliye waundia ni Saamiriyu (Msamaria). Naye akawaamrisha wamuabudu! Upumbavu gani huu wa akili zao! Hivyo wao walipo mfanya ndiye mungu wakamuabudu, hawakuona kuwa hawasemezi, wala hawezi kuwaongoa wafuate njia iliyo sawa? Hakika hawa wamejidhulumu nafsi zao kwa kitendo hichi kiovu.
Walipo tambua kuteleza kwao, na makaso yao, wakababaika, na wakajuta majuto makubwa kwa kumfanya ndama ndiye Mungu. Makosa yao yakabainika wazi, wakasema: Wallahi! Ikiwa Mola wetu Mlezi hakutusamehe hakika tutakuwa miongoni walio khasiri khasara iliyo dhaahiri; kwa vile kuabudu kisicho faa kuabudiwa.