Ewe Nabii! Wakumbushe hao waliopo miongoni mwao katika zama zako - ili iwe ni onyo kwa vile walivyo tenda walio watangulia - wakumbushe kauli yetu tulio waambia hao walio watangulia kwa ulimi wa Musa: Kaeni katika mji wa Baitul Muqaddas (Yerusalemu) baada ya kutoka jangwani. Na kuleni kheri zake kokote humo mtakako, na semeni: Tunakuomba ewe Mola Mlezi wetu, utufutie makosa yetu. Na muingie kwenye lango la mji kwa kuinamisha vichwa kama kurukuu kwa kumnyenyekea Mwenyezi Mungu. Mkifanya hivyo tutakufutieni dhambi zenu, na tutazidisha thawabu za watendao mema.