Na hawa makafiri wakiambiwa: Njooni kwenye yale aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu katika Qur'ani, na aliyo yaeleza Mtume, ili mpate kuongoka kwa kuyafuata, wao husema: Yanatutosha tuliyo wakuta nayo baba zetu. Yawafalia hawa kusema hayo? Ijapo kuwa hao baba zao ni kama nyama hoa, hawajui lolote la haki, wala hawaijui njia ya kuendea yaliyo sahihi.
Enyi mlio amini! Fanyeni pupa ya kwendea kwenye matengenezo ya nafsi zenu kwa kumt'ii Mwenyezi Mungu. Upotovu wa mwengineo hautakudhuruni ikiwa nyinyi mmo kwenye uwongofu na mnalingania Haki. Na nyote nyinyi marejeo yenu ni Mwenyezi Mungu peke yake Siku ya Kiyama. Hapo atakupeni khabari ya vitendo vyenu, na kila mmoja wenu atamlipa kwa aliyo yatanguliza, na wala hapana hata mmoja atae shikwa kwa dhambi za mwenginewe.
Enyi mlio amini! Mmoja wenu anapoona alama za kukaribia mauti na akataka kuusia lolote basi kushuhudia wasia huo iwe: kushuhudia watu wawili waadilifu katika jamaa zenu, au watu wawili wengineo ikiwa mmo safarini na ishara za mauti zikatokea. Wazuieni wawili hao baada ya Swala wanapo kusanyika watu, na waape kwa jina la Mwenyezi Mungu wakisema: Hatubadilishi kwa kiapo chake kwa chochote, hata ikiwa ni kutufaa sisi au yeyote katika jamaa zetu. Wala hatutaficha ushahidi alio tuamrisha Mwenyezi Mungu kuutimiza baraabara. Kwani tukificha ushahidi au tukasema lisio la kweli, tutakuwa miongoni mwa wenye kudhulumu na kustahiki adhabu ya Mwenyezi Mungu.
Na ikionekana kuwa mashahidi wawili hao wamesema uwongo katika ushahidi wao, au wameficha kitu, basi walio na haki zaidi kushika mahala pao ni wawili wengine walio karibu zaidi kukhusika na warithi wa maiti. Hao washike pahala pao baada ya Swala, wadhihirishe uwongo wa walio tangulia, na waape kwa Mwenyezi Mungu kuwa wale mashahidi wa mwanzo walisema uwongo, na: Yamini yetu inafaa zaidi kuliko yamini ya wale, na wala hatuitupi haki katika yamini zetu, wala hatuwatuhumu mashahidi wale kwa uzushi. Kwani tukifanya hivyo tutakuwa katika walio dhulumu, wenye kustahiki adhabu ya mwenye kumdhulumu mwenginewe.
Hukumu hii ndiyo njia ya karibu mno ya kuwezesha mashahidi watoe ushahidi ulio sawa kwa kuhifadhi kiapo chao kwa Mwenyezi Mungu, au kwa kuogopa kufedheheka kwa kudhihiri uwongo wao, pindi ikiwa warithi watakula yamini kupinga kiapo chao. Nanyi mumuangalie sana Mwenyezi Mungu katika viapo vyenu na amana zenu, na zit'iini hukumu zake, na muwe radhi nazo. Kwani katika hayo ndiyo yanapatikana maslaha yenu. Na msikhalifu hukumu za Mwenyezi Mungu, msije kutoka kwenye ut'iifu wake, kwani Yeye hamnafiishi kwa uwongzi wake mwenye kutoka katika ut'iifu wake.