Sifa zote nzuri ni haki ya Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye Mwenye kuumba, na Mwenye kumiliki, na Mwenye kupanga vyote vilioko mbinguni, na vilioko katika ardhi. Na Yeye peke yake ndiye Mwenye sifa Akhera, kwa kutamalaki kwake kuliko enea. Naye ndiye Mwenye hikima asiye kosa, Mwenye khabari zote, hapana asicho kijua siri yake.
Anajua kila kinacho ingia katika sehemu za ardhi, kama maji, na khazina, na vilio zikwa, na sehemu za maiti; na kila kinacho toka, kama wanyama, na mimea, na maadeni, na maji ya visima, na chemchem. Na anajua vinavyo teremka kutoka mbinguni, kama Malaika, na Vitabu wanavyo vipokea Manabii, na mvua, na radi; na anajua vinavyo panda ndani yake na kwendea huko, kama Malaika, na a'mali za ibada, na roho. Na Yeye ni Mwingi wa rehema, Mkubwa wa kusamehe.
Na wenye kukufuru wakasema: Haitujii Saa iliyo ahidiwa kuwa ni ya kufufuliwa na kukusanywa watu. Waambie ewe Mtume! Hapana shaka itakujieni, nami naapa kwa Mola wangu Mlezi, Mwenye kujua ya siri, ambaye hapana chenye kughibu na ujuzi wake hata ingawa kiasi ya chembe tu, si katika mbingu wala katika ardhi. Wala kilicho kidogo kuliko chembe, wala kikubwa kuliko hivyo hakikosi kuandikwa katika Kitabu kilicho timia, chenye kubainisha kila kitu. Dharra , tuliyo ifasiri "Chembe", na kisayansi ni Atom kwa hakika katika lugha ya Kiarabu ni kitu kidogo sana, kama sisimizi mdogo, au chembe ya vumbi. Na uzito wa Dharra maana yake ni uzani wake. Na Aya inaonyesha kuwa kipo kilicho kuwa ni kidogo kuliko Dharra. Na yafaa kutaja hapa kuwa sayansi za sasa zimethibitisha kuwa Dharra, yaani Atom, imegawika katika sehemu ndogo zaidi nazo ni Nucleus na Electrons. Na haya haya hayakuthibitika ila katika karne ya ishirini ya kuzaliwa Nabii Isa.
Ili Mwenyezi Mungu awathibitishe walio amini na wakatenda mema kwa ajili ya nafsi zao na kwa ajili ya watu wengine. Hao Waumini watendaji watapata kwa Mwenyezi Mungu msamaha wa kuwafutia madhambi yao, na riziki kunjufu isiyo na masimbulizi ndani yake.
Na hao walio zishughulisha nafsi zao kuipiga vita Qur'ani kutaka kuishinda amri ya Mwenyezi Mungu katika kumsaidia Mtume wake, hao watapata adhabu katika adhabu za mwisho wa ubaya na uchungu.
Na walio neemeshwa na Mwenyezi Mungu kwa kupewa ujuzi kuwa Qur'ani ulio teremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi, yenye ndani yake mambo ya itikadi na uwongofu, ni Haki isiyo kuwa na shaka yoyote, wanajua kuwa hiyo ndiyo yenye kuwaongoa watu kwendea Njia ya Mwenyezi Mungu, Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye kustahiki kila sifa njema.
Na makafiri waliambiana wenyewe kwa wenyewe, kwa kufanyia kejeli kufufuliwa: Je! Tukuonyesheni mtu ataye kuambieni kwamba mtapo kwisha kufa, na viwiliwili vyenu vikagawika mapande mapande kuwa ati mtafufuliwa tena kwa umbo jipya?