Wanaume wana haki ya kuwaangalia na kuwachunga wanawake, na kuwasimamia katika mambo yao kwa vile Mwenyezi Mungu amewapa wao wanaume sifa za kuweza kuisimamia haki hii, na kwa kuwa wao ndio wanao hangaika na kufanya juhudi ya kutafuta mali ya kuutumilia ukoo mzima. Basi wanawake wema wanakuwa ni wat'iifu kwa Mwenyezi Mungu na waume zao. Ni wenye kuhifadhi vyote ambavyo waume zao hawavioni kwa sababu Mwenyezi Mungu ameamrisha vihifadhiwe, na kwa kuwapa wao tawfiki. Na wanawake wanao onyesha kuanza uasi wanasihini kwa maneno yenye kuathiri. Kama hawakusikia tenganeni nao kitandani. Hawakusikia, watieni adabu kwa pigo dogo, si la kuwajuruhi wala kuwadhalilisha. Wakirejea kwenye ut'iifu wenu kwa njia mojapo katika hizi tatu basi msiwatafutie kisababu cha kuwatesa zaidi kuliko haya. Hakika Mwenyezi Mungu yuko juu yenu, naye atakupatilizeni pindi mkiwaudhi wake zenu au mkawafanyia jeuri.
Pindi pakitokea kukhitalifiana baina ya mke na mume, na mkakhofia kutokea kufarikiana kutako leta t'alaka, chagueni waamuzi wawili. Mmoja kutokana na upande wa mume na mwengine upande wa mke. Wakitaka kusuluhiana Mwenyezi Mungu atawawafikisha wafikilie lilio kheri kwa wote wawili, nako ama kukaa kwa wema au kuachana kwa ihsani. Hakika Mwenyezi Mungu anachungua kila kitu cha waja wake, kilicho dhihiri na kilicho fichikana.
Nanyi muabuduni Mwenyezi Mungu peke yake, wala msimfanyie washirika katika Ungu na kuabudiwa. Na watendeeni wema wazazi wenu bila ya taksiri yoyote, na pia jamaa zenu, na mayatima, na walio fakirika kwa sababu ya kuemewa au kupata masaibu katika mali yao, na jirani mliye karibiana naye kwa nasaba, na jirani mtu mbali, na mwenzio katika kazi au njia au majlisi, na msafiri mhitaji asiye kuwa na kituo katika nchi maalumu, na watumwa wenu wanaume na wanawake mlio wamiliki. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi anaye jipa ubora juu ya watu wengine, na hawachukulii watu kwa huruma, na anakithirisha kujisifu mwenyewe kwa kujifakhiri.
Hao ndio wanao ongeza juu ya takaburi na tafakhuri yao ila ya kuwafanyia watu ubakhili kwa mali yao na juhudi yao. Tena ikawa wanawataka watu wafanye ubakhili kama wao. Kazi yao ni kukhofia neema na fadhila ya Mwenyezi Mungu isiwatoke. Kwa hivyo, basi, hawajifai wenyewe wala hawawafai watu. Wapinzani kama hao tumekwisha waandalia adhabu ya kutia machungu na ya kudhalilisha.