Basi hapana aliye dhaalimu mkubwa zaidi kuliko yule anaye msingizia Mwenyezi Mungu lisio kuwa lake, na akaikanusha Haki bila ya kufikiri wala kuzingatia pale inapo mjia kwa ndimi za Mitume. Kwani katika Jahannamu sio makaazi ya makafiri walio ghurika hata wakamfanyia jeuri Mwenyezi Mungu?
Wachamngu hao watapata kutoka kwa Mola wao Mlezi kila wakipendacho. Fadhila hiyo ni malipo ya kila mwenye kufanya vizuri katika itikadi yake na vitendo vyake.
Mwenyezi Mungu amewakirimu wachamngu kwa alivyo wakirimu, ili awafutie vile vitendo vyao viovu kabisa, na awalipe ujira wao kwa bora ya vitendo vyao walivyo vitenda duniani.
Mwenyezi Mungu, peke yake, ni Mwenye kuwatosheleza waja wake kwa kila lilio wakhusu. Na ati hao makafiri wa Kikureshi wanakutisha, ewe Muhammad, kwa miungu yao wanayo iomba badala ya Mwenyezi Mungu. Na hayo ni katika upotovu wao. Na mwenye kupotozwa na Mwenyezi Mungu, kwa kumjua kuwa huyo amekhiari upotovu kuliko uwongofu, basi hatakuwa na mwongozi wa kumwongoza.
Na mwenye kuongozwa na Mwenyezi Mungu kuendea Haki, na akamwezesha kuifikia, kwa kujua kwake kuwa huyo amekhiari uwongofu kuliko upotovu, basi hatokuwapo wa kumpotoa akaiacha Njia ya Uwongofu. Kwani Mwenyezi Mungu si ndio Yeye ambaye hashindiki kwa kila upande, ambaye ni Mwenye kulipiza kwa ukali? Na kwa hivyo huwalinda vipenzi vyake na maadui wake?
Na ninaapa, lau ungeli wauliza, wewe Muhammad, hawa washirikina: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka wangeli sema: Mwenyezi Mungu ndiye aliye ziumba. Ewe Muhammad, waambie: Mmezingatia mkawaona hao miungu mnao washirikisha na Mwenyezi Mungu, wanaweza kuniondolea madhara ikiwa Mwenyezi Mungu anataka kunidhuru? Au wanaweza kunizuilia rehema yake akitaka inifikie? Ewe Muhammad! Waambie: Anaye nitosheleza kwa kila kitu ni Yeyey peke yake, si mwenginewe, ndiye Yeye wanaye mtegemea wote wanao tegemea na kumwachilia kila kitu.
Waambie, kwa kuwapa ahadi: Enyi watu! Ishikilieni hiyo hiyo njia yenu ya ukafiri na kukadhibisha, na mimi hakika ninashikilia aliyo niamrisha Mola wangu Mlezi. Mtakuja ona nani katika sisi atakaye fikiwa na adhabu ya kumdhalilisha, na atakaye teremkiwa na adhabu ya daima isiyo mwondokea?
Waambie, kwa kuwapa ahadi: Enyi watu! Ishikilieni hiyo hiyo njia yenu ya ukafiri na kukadhibisha, na mimi hakika ninashikilia aliyo niamrisha Mola wangu Mlezi. Mtakuja ona nani katika sisi atakaye fikiwa na adhabu ya kumdhalilisha, na atakaye teremkiwa na adhabu ya daima isiyo mwondokea?