Kwani watu wote ni sawa? Mwenye kufunguliwa kifua chake na Mwenyezi Mungu kwa Uislamu kwa kupokea mafunzo yake, na akawa na utambuzi unao tokana na Mola wake Mlezi, huyo basi ni kama yule anaye kataa kuangalia Ishara zake? Basi hao ambao nyoyo zao zimekuwa ngumu hata hawamkumbuki Mwenyezi Mungu watapata adhabu kali! Hao wenye nyoyo ngumu wameitupa Haki iliyo wazi.
Mwenyezi Mungu ameteremsha hadithi nzuri kabisa, nayo ni Kitabu ambacho zimeshabihiana maana zake na matamko yake kwa kufikilia ukomo wa kuwashinda watu kuleta mfano wake, na hukumu zake. Mawaidha na hukumu zinakaririwa, kama kunavyo kaririwa kusomwa kwake. Kinapo somwa Kitabu hicho na kikasikiwa maonyo yake, ngozi za wenye kumkhofu Mola wao Mlezi hukunjika, na kisha hulainika ngozi zao na nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Hicho Kitabu kilicho kusanya sifa hizi ni Nuru ya Mwenyezi Mungu ambayo kwayo humwongoa amtakaye, ikamwezesha kufikilia kumuamini Yeye. Na anaye achwa na Mwenyezi Mungu apotee kwa kumjua kuwa tangu hapo ataiacha Haki, basi hapati mwongozi wa kumwokoa na upotofu wake.
Kwani watu wote ni sawa? Mwenye kuikinga adhabu ovu, kali, kwa uso wake Siku ya Kiyama baada ya kuwa mikono yake imetiwa pingu, ni kama anaye kuja kwa amani Siku ya Kiyama? Na wenye kudhulumu wataambiwa: Onjeni laana ya vitendo vyenu!
Mwenyezi Mungu akawaonjesha unyonge katika maisha ya duniani. Ninaapa: Hakika adhabu ya Akhera ni kubwa zaidi kuliko ya duniani, lau kwamba walikuwa ni watu wa kujua na kuangalia!
Na bila ya shaka tulikwisha wabainishia watu katika hii Qur'ani kwa kila mfano wa kuwakumbusha Haki, kwa kutaraji kuwa watakumbuka na watawaidhika.
Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mshirikina kama mtumwa aliye milikiwa na watu kadhaa wenye kushirikiana, na wenye kumgombania. Na mfano wa mwenye kuamini Mwenyezi Mungu Mmoja kama mtu ambaye amemilikiwa na mtu mmoja tu. Je hao wanakuwa sawa? Alhamdulillahi kwa kusimama hoja mbele ya watu. Lakini watu wengi hawaijui Haki.