Ikiwa kutoa kusaidia mayatima na masikini na wengineo ni kuhami jamii ya umma kwa ndani, kadhaalika kupigana vita ni kuuhami umma na adui wa nje. Kwa hivyo enyi Waislamu, mmelazimishwa kupigana vita kuhami Dini yenu, na kulinda nafsi zenu. Hakika hizo nafsi zenu kwa mujibu wa tabia zake zinachukia mno kupigana. Lakini huenda mkachukia kitu na ndani yake ipo kheri kwenu, na mkapenda kitu na ikawa ipo shari kwenu. Na Mwenyezi Mungu anayajua maslaha yenu ambayo yamefichikana, na nyinyi hamyajui. Basi tendeni mlilo amrishwa kulitenda.
Waislamu walichukia kupigana katika mwezi mtakatifu, ndio wakakuuliza juu yake. Waambie: Naam, kupigana katika mwezi mtakatifu ni dhambi kubwa. Lakini kubwa zaidi ni haya wayatendayo maadui zenu nayo: kuwazuia watu wasifuate Njia ya Mwenyezi Mungu, wasende kwenye Msikiti Mtakatifu, na kuwafukuza Waislamu kutoka Makka. Na hayo maudhi na mateso yao kuwafanyia Waislamu ili waache Dini yao ni makubwa zaidi kuliko mauwaji yoyote. Kwa hivyo imehalalishwa kupigana vita katika mwezi mtakatifu kwa ajili ya kupambana na maovu haya. Hichi ni kitendo kikubwa cha kujikinga na lilio kubwa zaidi. Enyi Waislamu! Jueni kuwa mwendo wa watu hawa ni mwendo wa ukhalifu na udhaalimu. Na wao hawakubali kwenu uadilifu wala mambo ya kiakili. Na wala hawatasita kukupigeni vita mpaka wakuachisheni Dini yenu pindi wakiweza. Na atakaye dhoofika kwa mashambulio yao akaacha Dini yake na akafa katika ukafiri, basi watu kama hao watapoteza vitendo vyao vyema vyote vya duniani na Akhera. Na hao ni watu wa Motoni ambako watadumu.
Wenye kuamini imani ya kweli hata wakahama kwa ajili ya kuinusuru Dini na kwa ajili ya Jihadi ili Dini ienee hao wanangojea thawabu kubwa za Mwenyezi Mungu. Na ikiwa wamefanya kasoro kitu basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, anasamehe dhambi, Mwenye kurehemu, anawarehemu waja wake kwa uwongofu na kuwalipa.
Ewe Muhammad! Wanakuuliza juu ya hukumu ya ulevi na kamari. Waambie kwamba katika yote mawili hayo pana madhara makubwa, kwa kuharibu siha na kupoteza akili na mali, na kuleta chuki na uadui baina ya watu. Pia ndani ya hayo yapo manufaa, kama kujipumbaza na kupata faida ya sahali. Lakini madhara yake ni makubwa zaidi kuliko manufaa yake, basi epukaneni nayo. Na wanakuuliza watoe nini? Wajibu watoe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kilicho chepesi na hakina uzito kukitoa. Hivyo ndio Mwenyezi Mungu anakubainishieni Aya zake mpate kufikiri yale yatakayo kurejeeni katika maslaha ya dunia na Akhera. Kifungu hichi cha Qur'ani kinatuwekea wazi makusudio ya sharia ya Kiislamu. Kinatueleza kuwa sharia inataka manufaa ya waja. Chenye kuzidi nafuu yake kuliko madhara kinafaa. Chenye nafuu chache kuliko madhara kinakatazwa. Pia kifungu kinatuonyesha kuwa vitu ulimwenguni vimechanganya mema na mabaya. Hapana ovu lisio kuwa na wema, wala wema usio na uovu. Ulevi, mama wa maovu, unao haribu akili na kumfanya mtu kuwa mnyama, nao una faida pamoja na uovu wake usio na mpaka. Na kamari inayo shughulisha nafsi na akili, ikaleta mpapatiko usio sita, nayo ina nafuu yake pamoja na kuwa na madhambi yanayo fisidi maisha na nyumba za watu, na kila makhusiano bora ya binaadamu.