Watu wamekithirisha maneno juu ya Kibla kama kwamba wema wote ni hayo tu. Hivi sivyo. Kuelekea upande fulani, mashariki au magharibi, sio msingi wa Dini na kupata kheri, lakini kupata wema ni mambo kadhaa wa kadhaa, baadhi yake ni nguzo za itikadi sahihi, na baadhi yake ni katika misingi ya tabia njema na ibada. La kwanza: kumuamini Mwenyezi Mungu, na Siku ya kufufuliwa na kukusanywa na kuhisabiwa na yatakayo tokea Siku ya Kiyama; na kuamini Malaika, na Vitabu vilivyo teremka kwa Manabii, na kuwaamini wenyewe Manabii. Na pili: kutoa mali kwa kupenda na kuridhia nafsi kuwapa mafakiri katika jamaa, na mayatima, na wenye shida ya haja, na wasafiri walio katikiwa safari yao wasipate cha kuwafikishia wendako, na walio lazimika kuomba kwa haja walio nayo, na kukomboa watumwa. ( Walio fungwa na kutawaliwa na dhaalimu ni watumwa pia. )Tatu: kushika Swala. Lane: kutoa Zaka iliyo lazimishwa. La tano: kutimiza ahadi bilhali wal maal. La sita: kustahamili maudhi yanayo teremkia roho na mali, mnapo pambana na adui zama za vita. Basi wenye kukusanya imani hizi na vitendo hivi vya kheri ndio walio sadikisha Imani yao, na wao ndio wanao jilinda na ukafiri na mambo machafu na wakayaepuka.
Katika Sharia tulizo walazimisha Waumini ni hukumu za mauwaji ya makusudi. Tumewaandikia kisasi kwa mauwaji. Na wala msichukulie dhulma za kijahiliya , walipo kuwa wakimuuwa muungwana asiye uwa kwa ajili ya mtumwa, na wakimuuwa mwanamume asiye uwa kwa ajili ya mwanamke, na mkuu asiye uwa badala ya mwenginewe aliye uwa, akaachiliwa aliye uwa khasa. (Kwa kila ukoo kujiona bora). Yatakikana yule aliye uwa auwawe yeye, akiwa ni muungwana, au mtumwa, au mwanamke. Msingi wa sharia ya kisasi ni kuondoa kufanyiana uadui kwa kumuuwa yule yule aliye uwa ili kuuzima moto wa kulipizana na kuondoa uadui. Walio uliwa mtu wao wakiacha kisasi, wakapendelea kuwasamehe wenzao, watakuwa na haki ya kupewa fidia kwa maiti wao. Na wao inatakikana wawe wasemehevu bila ya kumkahirisha aliye uwa. Na juu ya mwenye kuuwa alipe fidia bila ya kujikurupusha. Katika hukumu ya mauwaji kama tulivyo ilazimisha pana wepesi kwa Waumini ukilinganisha na hukumu ya Taurati inayo lazimisha kisasi tu, na kama ilivyo kuwa ni rehema ukilinganisha na watakavyo wenginewe kuwa muuwaji aachiliwe bure bila ya kumtaaradhi. Basi mwenye kuivuka hukumu hii baada ya hayo atapata adhabu chungu duniani na Akhera. Waarabu zama za jahiliya walikuwa hawafanyi usawa baina ya watukufu na wanyonge. Akiuliwa mwongozi hawatosheki na kumuuwa muuwaji bali huyo huachwa akenda kulipizwa kisasi kwa mwongozi wa kabila ya muuwaji. Kwao roho si sawa, na damu si sawa. Uislamu haukukubali haya, lakini ukapasisha Kisasi, roho kwa roho, mwenye kuuwa huuwawa. Muuwaji yeyote awaye atauliwa akiwa muungwana, mtumwa au mwanamke. Haya ni kwa ajili ya usawa katika damu; hapana mwenye damu tukufu na damu isiyo tukufu. Na inafahamika kwa ishara kuwa nafsi kwa nafsi. Na hii ni sharia ya milele, ilikuwako katika Taurat, na Injil na Qur'ani. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: "Na tuliwaandikia kuwa nafsi kwa nafsi..." (taz. sura Almaida ). Na Mtume s.a.w. amesema: "Damu za Waislamu ni sawa." Na amesema: "Nafsi kwa nafsi". Zingatia: Uislamu kwa sharia ya kisasi ina nadhari nyengine, sio kama kanuni za kutungwa. Imewapa wenye kuuliwa mtu wao haki ya kutaka muuwaji auwawe, kuondoa fitna na umwagaji wa damu mkubwa. Imewapa haki ya kusamehe au kulipwa kisasi, wala haizuilii serikali kumfedhehi aliye uwa ikiona hivyo ni maslaha. Uislamu hauzingatii sababu ya kuuwa, kwani mwenye kuuwa amedhulumu hata ikiwa sababu gani. Na huenda ukitafuta sababu akaonewa huruma mkosa, na kumpuuza mkoswa. Na hayo hupelekea mchafuko wa watu kuchukua kisasi mkononi mwao, na kuzalikana makosa juu ya makosa ya kuuwa, kwa kutoridhika wale walio uliwa mtu wao. Nadharia hii ya Kiislamu sasa inadurusiwa katika vyuo vikuu vya Ulaya.
Hakika rehema ya Mwenyezi Mungu kwenu ni kubwa kwa hii hukumu ya kisasi. Kwa fadhila ya kisasi jamii yenu ina hakika kupata maisha ya amani na salama. Haya ni kwa kuwa mwenye kutaka kuuwa akijua kuwa naye atauwawa atajizuia kutenda alilo kusudia. Kwa hivyo yeye na yule ambaye angeli uwawa wanahifadhika. Lakini ikiwa kama ilivyo kuwa zama za ujahili akiuliwa mkuu kwa kuuliwa mtu mdogo, na asiye na kosa badala ya mwenye makosa - hapo inakuwa ni kuzua fitna, na kuondoka utulivu na amani. Wenye akili nawazingatie faida ya sharia ya kisasi. Hayo yatawapelekea watambue upole wa Mwenyezi Mungu kwao kuendea njia ya uchamngu, na kuzifuata amri za Mwenyezi Mungu Subhanahu.
Kama tulivyo weka sharia ya kisasi kwa maslaha ya umma na kuhifadhi jamii, vile vile tumeleta sharia ya maslaha ya ukoo na kuulinda, nayo ni Sharia ya Wasiya. Basi mwenye kuona kuwa amekabiliwa na mauti naye akawa na mali basi yatatikana awawekee katika mali yake fungu la wazazi wake na jamaa zake, wale jamaa ambao hawamrithi. Katika hayo afuate mwendo unao pendeza na unakubaliwa na wenye akili. Asiwe akampa tajiri na akamwacha fakiri, bali amfadhilishe yule mwenye haja zaidi, wala asiweke sawa ila wale wenye pato sawa. Na faridha hiyo ni haki iliyo mwajibikia mwenye kupenda uchamngu na kufuata amri za Dini.
Ukitoka wasiya basi huo ni haki iliyo waajibu, haijuzu kuugeuza na kuubadilisha ila ikiwa wasiya huo umeacha uadilifu. Mwenye kubadilisha haki akageuza wasiya muadilifu ulio sawa baada ya kujua hukumu hii basi huyo amepanda madhambi yatakayo mletea adhabu. Mwenye kuusia hana kosa kwa yatakayo tokea baada yake, wala hakudhani kuwa atakuwapo atakaye fanya hayo, wala yeye hapatilizwi kwa hayo. Mwenyezi Mungu, hakika, ni Mwenye kusikia na kujua, wala hapana linalo fichikana kwake.