Alif, Lam, Raa. Hizi harufi na mfano wake, zinazo fanya maneno yenu, enyi Waarabu, ndizo hizo hizo zinazo fanya Aya za hichi Kitabu, ambacho ni muujiza unao waemea watu kuuiga. Muujiza ulio wazi unao fafanua kwa kila mwenye kutafuta uwongozi ndani yake, na uwongofu. Na kwa hizi harufi za kutamkika zikasikilizana sauti yake wanazinduliwa watu watanabahi. Basi wasikilize, ijapo kuwa waliwafikiana kuwa wasisikilize.
Sisi tunakusimulia, ewe Nabii, visa vizuri kabisa kwa kukufunulia Kitabu hichi. Na kabla ya haya ulikuwa umeghafilika nayo, huyajui, haya, wala mawaidha yaliomo ndani yake, na Aya zake zilizo wazi.
Katika visa hivi, ewe Nabii, kipo hichi kisa cha Yusuf, pale alipo mwambia baba yake: Ewe babaangu! Hakika mimi nimeona usingizini nyota hidaa'shara, (kumi na moja) na jua, na mwezi. Nimeona vyote hivyo vikininyenyekea, vikisujudu mbele yangu. Yusuf, Alayhi Ssalam, alikuwa mwana wa Yaaqub, Muabrani, Mkanaani. Akauzwa Misri katika enzi ya utawala wa wavamizi wa kigeni waitwao Wahiksos. Na kwa ionekanavyo hao Wahiksos ni katika kabila za Kisami walio ingia Misri kutoka Sham wakaiteka Delta ya Misri mnamo mwaka 1730 k.k. ( kabla ya Nabii Isa a.s.) na kabla ya kumalizika enzi ya ukoo wa kumi na tatu wa Mafirauni. Wakaihukumu Misri kwa muda wa karne unusu. Wakafukuzwa mnamo mwaka 1580 k.k. na Ahmas wa Mwanzo aliye anzisha ukoo wa 18. Wakatolewa nje ya mipaka ya Misri.