Qaaf. Hii ni harufi katika harufi za alifbete iliyo fungulia Sura hii kama ilivyo ada ya Qur'ani katika kufungulia Sura kadhaa wa kadhaa kwa harufi kama hii, ili kuwakabili makafiri kama wanaweza kuleta mfano wake, na pia kuwazindua watu wasikilize yanayo somwa. Ninaapa kwa Qur'ani yenye ubora, na utukufu, na hishima kwamba hakika Sisi tumekutuma wewe, ewe Muhammad, ili uwaonye watu kwa hii.
Bali walistaajabu kutokea Mtume miongoni mwa jinsi yao akiwaonya kuwa watafufuliwa. Makafiri wakasema: Jambo hili hatulijui, na la ajabu!
Sisi hakika tunajua vipi ardhi inavyo vimeza viwiliwili vyao baada ya kufa. Na Sisi tunacho Kitabu kinacho dhibiti na kuhifadhi kila kitu hata kidogo.
Wao hawayazingatii aliyo kuja nayo Mtume, bali walimkadhibisha mara tu bila ya kuzingatia na kufikiri. Basi wao wamo katika hali ya kubabaika, hawana utulivu.
Wameghafilika hata hawaitazami mbingu ilivyo nyanyuliwa juu yao bila ya nguzo? Vipi tumetengeneza ujenzi wake, na tukaipamba kwa nyota, na haina nyufa za kuitia kombo! Mbingu ni kote kulio juu yetu, na ndani yake vimo vitu vya namna mbali mbali, vinaogelea katika njia zao, nyota na sayari. Na hayo ni kwa nidhamu ya uangalizi mkubwa, na mshikamano ulio timia, na vilevile zinafuata kwa mpango wake kuwafikiana na kanuni za mvutano, basi hazitelezi.
Na ardhi tumeikunjua na tukaisimamisha milima iliyo kaa imara na kuthibiti kwenda chini. Na tukaijaalia kumea kila namna ya mimea mizuri ya kuwafurahisha watazamao. Gamba lilio funika ardhi katika mwahali maalumu limetuna, ndio hiyo milima. Na pengine limedidimia ndio sakafu ya chini ya bahari. Na uzani wa vitu hivi vizito vinalingana wenyewe kwa wenyewe. Na ni katika uwezo wa Mwenyezi Mungu na hikima yake kupatikana kulingana huku kwa uzani, na ukawa umethibiti kwa kupenya madda za ardhi zilizo fanyika hilo gamba jembamba chini ya mat'abaka ya juu juu. Na hayo ni kutoka kuliko kuwa kuzito kwendea kuliko kwepesi.
Na kutoka mbinguni tukateremsha maji yenye kheri nyingi na baraka, na kwa hayo tukaotesha mabustani yenye miti, na mauwa, na matunda, na tukatoa kwa hayo nafaka za makulima ya kuvunwa.
Tumeotesha hiyo ili iwe ni riziki kwa waja wetu, na tukaihuisha kwa maji ardhi iliyo kauka mimea yake. Hali kadhaalika ndivyo kufufuliwa wafu kutoka makaburini.
Kabla ya hawa, kaumu nyingi ziliwakadhibisha Mitume- kaumu ya Nuhu, na kaumu nyengine iliyo kuwa ikiitwa "Watu wa Rassi", na wa Thamudi, na wa A'di, na wa Firauni, na kaumu Lut'i, na kaumu iliyo kuwa maarufu kwa jina la "Watu wa Machakani", na kaumu ya Tubbaa' - wote hao waliwakadhibisha Mitume wao. Kwa hivyo wakastahiki maangamizo niliyo waahidi.
Na kaumu iliyo kuwa maarufu kwa jina la "Watu wa Machakani", na kaumu ya Tubbaa' - wote hao waliwakadhibisha Mitume wao. Kwa hivyo wakastahiki maangamizo niliyo waahidi.
Kwani kutaka kwetu kulipungua, au uwezo wetu ulitetereka, hata tukashindwa kwa kule kuumba kwa mara ya kwanza, tusiweze tena kuwarejeza? Hasha! Hatukushindwa, nao wanatambua hayo. Bali wao wana shaka tu na wanadanganyikiwa na huku kuumbwa kupya baada ya kufa.