Kitabu hichi ni namna ya peke yake kwa uzuri wake kwa matamshi na ibara yake ya utungaji, na kwa maana inavyo pambanua baina Haki na baat'ili, na bishara na onyo, na kuzitengeneza nafsi, na kupiga mifano, na kubainisha hukumu. Nacho kinasomwa kwa ulimi wa Kiarabu, chepesi kukifahamu kwa watu wanao jua.
Chenye kuwapa khabari njema Waumini wenye kutenda kuwa watapata neema iliyo andaliwa kwa ajili yao, na kuwakhofisha wanao kanusha kuwa watapata adhabu chungu iliyo andaliwa kwa ajili yao. Lakini wengi walikitupilia mbali, wala wasinafiike nacho, kama kwamba hawakusikia.
Na makafiri wakamwambia Mtume s.a.w.: Nyoyo zetu zimo katika vifuniko vizito kwa hayo unayo tuitia yaliyo khusu Tawhidi (Upweke) wa Mwenyezi Mungu. Na masikioni mwetu mna uziwi, basi hayasikii hayo unayo tulingania. Na baina yetu na wewe lipo pazia nene linalo tuzuia kukubali hayo uliyo tuletea. Basi fanya utakalo, na sisi tunafanya tutakalo.
Ewe Mtume! Waambie: Hakika mimi si chochote ila ni mtu mfano wenu nyinyi, napata Wahyi (Ufunuo) kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwamba wa kuabudiwa kwa haki na nyinyi ni Mungu Mmoja tu. Basi fuateni Njia Iliyo Nyooka ya kwendea kwake! Na mtake kwake msamaha kwa madhambi yenu. Na washirikina wasio toa Zaka kuwapa wanao stahiki watapata adhabu kali. Na wao tu, si wenginewe, ndio wanao kataa kuwa upo uhai wa Akhera.
Ewe Mtume! Waambie hawa washirikina: Ama nyinyi mnastaajabisha! Mnamkataa Mwenyezi Mungu aliye iumba ardhi kwa siku mbili, na huku juu ya hayo, mnamfanyia washirika wa kushirikiana naye huyo Muumba ardhi, Mmiliki wa walimwengu wote na Mlezi wao? Zimetajwa Siku moja au Siku nyingi katika Sura nyengine. Katika Surat Al-Hajj, Aya 47 Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: "Na kwa hakika siku moja kwa Mola wako Mlezi ni kama miaka elfu mnavyo hisabu nyinyi." Na katika Surat Assajdah, Aya 5 amesema Mtukufu: "Anapitisha mambo yote yaliyo baina ya mbingu na ardhi, kisha yanapanda kwake kwa siku moja tu ambayo kipimo chake ni miaka elfu mnayo hisabu." Na katika Surat Al-Ma'arij Mtukufu amesema: "Malaika na Roho hupanda kwake katika siku iliyo kadiri yake ni miaka elfu khamsini." Maoni ya kitaalamu: Vipimo vya wakati wanavyo vitumia watu vimefungamana na dunia na inavyo zunguka juu ya msumari-kati wake na kulizunguka jua. Mtu akitoka kwenye ardhi (dunia) akenda kwenye sayari nyengine za mbinguni vipimo hivyo vya nyakati vinabadilika kwa kuzidi au kwa kupungua. Na hizi Aya tukufu zinaonyesha ishara ya ukweli huu wa ki-ilimu, na ya kwamba zama au nyakati ni jambo la mlinganisho tu. Na bila ya shaka ipo miaka ya ki-ilimu ya Falaki ya kulinganisha yenye kumkinika kuifarikisha baina yao. Mwaka wa ki-jua wa duniani huhisabiwa kwa kupimwa wakati ambao dunia inachukua kulizunguka jua kwa ukamilifu mnamo siku 365, na ilhali sayari zilio karibu na jua kama U't'aarid (Mercury) humaliza safari yake ya kulizunguka jua mnamo siku 88, na upande mwengine sayari ya Blutu (Pluto) ambayo ndiyo sayari iliyo mbali mno na jua, na ndiyo inazunguka taratibu mno inachukua kuzunguka kwake mnamo miaka 250 kwa mujibu wa miaka yetu sisi.
Naye Mwenyezi Mungu amesimamisha juu ya ardhi milima iliyo simama imara ili isiyumbe nanyi; na akakithirisha humo kheri nyingi, na akakadiria humo riziki kwa watu wake, kwa mujibu wa hikima yake, mnamo siku nne. Na nyinyi, juu ya haya, mnakwenda kumwekea washirika? Na Yeye amekadiria kila kitu bila ya upungufu wala kuzidi. Kufafanua huku katika uumbaji wa ardhi na vilio juu yake ni maelezo kwa hao wanao uliza.
Kisha amekhusisha uweza wake na kuumba mbingu, nazo zilikuwa kama moshi, basi zikawapo. Na kuumba kwake mbingu na ardhi kwa mujibu wa mapendo yake ni jambo jepesi kwake, ni kama kukiambia kitu: Njoo ukipenda usipenda, nacho kikat'ii.